.

.

.

.

Thursday, June 25, 2009

AFANANISHA MAWAZIRI KAMA MBWA

Na Martin Malera, Dodoma


MASHAMBULIZI ya wabunge dhidi ya mawaziri bungeni, yamefikia katika hatua mbaya zaidi baada ya Mbunge wa Iramba Magharibi, Juma Kilimba (CCM), kuwafananisha na mbwa.
Kilimba aliwafananisha mawaziri na mbwa juzi usiku alipokuwa akichangia hotuba ya Waziri Mkuu ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2009/2010 inayotarajiwa kuhitimishwa leo.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu, tutakunong’oneza mawaziri hawa kama mbwa, maana mbwa anamuheshimu sana anayempa chakula na si anayemtafutia chakula, wanaheshimu sana walio juu yao kikazi badala ya kuwaheshimu wananchi,” alisema Kilimba.
Kilimba alisema kuna mawaziri wamekuwa wakiwagawa wabunge kwa misingi ya ukanda, urafiki na muonekano.
Kwa mujibu wa Kilimba, amekuwa akiwapelekea mawaziri hao shida za jimboni kwake, lakini majibu anayopewa hayaridhishi na kadiri siku zinavyokwenda, ndivyo mambo yanavyozidi kuwa mabaya.
“Inashangaza unakwenda kwa waziri kumpelekea kero, anajibu ana watu milioni 40, kila mtu anamuangalia yeye, kama hawezi aondoke aende nyumbani kwake.
Kilimba aliwataka mawaziri hao kutambua kuwa yeye hapeleki matatizo yake binafsi bali ya wananchi waliomchagua na kuongeza kuwa, nia ya mawaziri hao ni kuwaharibia kazi wabunge kwa wapiga kura wao.
“Mawaziri hawa wako radhi kusafiri nje ya nchi hata mara nne, ukiwaambia twende Iramba wanauliza barabara zenu ziko salama?” alisema Kilimba.
Wakati Kilimba akiwafananisha mawaziri na mbwa, Mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama (CCM), ambaye ni Mwenyekiti wa Bunge, amemponda Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia, kuwa hafai, si msikivu na anaishangaa serikali kuendelea kumwongeza mabilioni ya fedha kwa ajili ya mafuta wakati hataki kutembelea wilayani.
Mhagama alisema Ghasia si msikivu wa kero za wananchi, jambo ambalo limekuwa likiwafanya waendelee kupata shida ambazo zingeweza kupatiwa ufumbuzi.
Mhagama alisema kuna watumishi wanaofanya kazi serikalini katika wilaya zaidi ya 40, ambao hawako katika orodha ya malipo ya serikali na amefuatilia kwa Waziri Ghasia kwa miaka mitatu bila kupata majibu.
Alisema iwapo hatapatiwa majibu, atawashawishi wabunge wenzake wanaotoka katika wilaya hizo waungane na kuleta hoja binafsi bungeni ili wamalize tatizo hilo.
Mbunge huyo aliamua kupitia baadhi ya vipengele vya bajeti ya waziri huyo na kuhoji sh milioni 300 za mafuta alizowekewa waziri huyo wakati hafuatilii kero za wananchi, zinatumika kwa kazi gani wakati anakaa ofisini tu.
Hata hivyo, Mbunge wa Viti Maalumu, Lucy Owenya (CHADEMA), alipokuwa akichangia hotuba hiyo, aliwageuka wenzake waliokuwa wakiwajia juu mawaziri na kusema kuwa ni wanafiki.
“Hapa tuliapa kwa Biblia na Qurani, lakini hawa wanalalamika na kuwanyooshea kidole mawaziri kisha baadaye wanaunga mkono hoja,” alisema Owenya.

No comments:

Post a Comment