HALI imeendelea kuwa tete ndani ya klabu ya Simba baada ya viongozi wake wawili mwenyekiti Hassan Dalali na makamu wake Omary Gumbo kuanza kutupiana vijembe hadharani.
Mwenyekiti wa Simba, Hassan Dalali amemtuhumu makamu wake Omary Gumbo kuwa ana chembe chembe za Yanga, huku mchezaji huyo wa zamani wa wekundu hao akijibu mapigo kwa kusema mwenyekiti huyo 'amefilisika kimawazo.'
"Tatizo ana chuki kwa vile amenyang'anywa gari hapati tena fedha, mchuzi umeondoka, wote tutembee kwa miguu, aliyechoka aondoke..."
Aliongeza kuwa Gumbo ana chembe chembe za Uyanga kwani mwaka 1971 akiwa mchezaji Simba alihongwa shilingi 300 ili ajiunge na Yanga, lakini wazee walimzuia 'inawezekana bado ana chembe chembe za Uyanga ndio maana mechi zote za Simba na Yanga huwa haonekani uwanjani ina tia mashaka chembe chembe za Uyanga zinaonekana wazi.'
"Aliyezoea kula nyama ya mtu hawezi kuacha ataendelea kula, tunaelekea kipindi cha uchaguzi, wanachama wawe makini na watu wanaowachagua wasichague wenye chembe chembe za Uyanga kama Gumbo", alisema Dalali.
Dalali aliyasema hayo jana ikiwa ni siku moja tangu Gumbo alipotangaza hatambui tamasha la 'Simba Day' lililopangwa kufanyika siku ya nane nane, na limeandaliwa na watu wachache na kwamba kamati ya utendaji haitambui bonaza hilo.
Lakini Dalali alisema tamasha hilo lipo pale pale na kwamba wanachama na mashabiki wa Simba watavaa nguo nyekundu na litakuwa linafanyika kila mwaka kwa kuwa klabu hiyo imezaliwa upya.
"Mechi za tarehe 8 na 15 zimepangwa na kocha, si kamati ya utendaji, kiongozi anapokataa programu ya mwalimu hatufai,"alisema Dalali
"Kocha amesema, kamati ya utendaji haipangi mechi, jambo la busara angeuliza timu imeendaje Zanzibar?, imepelekwa na nani?, inakula nini?kama kweli anauchungu, lakini si kuhoji fedha zinatumikaje?, watu wamechanga milioni 30 kwa ajili ya kambi mbona haulizi? alihoji na kuongeza "Wenzetu mpaka leo hawajaenda Mwanza wamefulia".
Dalali alisisitiza tamasha la 'Simba day' lipo palepale na kuhoji kuwa wanaopinga mbona hawajaipinga mechi ya Simba na Mtibwa na ile ya African Lyon na kuwataka Wanasimba wasitumiwe na wajitokeze kwa wingi uwanjani kwa kuwa mbali na mechi pia kutakuwa na burudani ya bendi.
Wakati Dalali akisema hayo Makamu Mwenyekiti wake, Gumbo alidai Mwenyekiti ameishiwa kimawazo na hajui kitu chochote alichokuwa anaongelea kwani suala la kupewa fedha na Yanga ni yeye Gumbo aliyemwadithia.
''Huyo Dalali anasema mimi nina chembe chembe za Yanga kwa kuwa niliwahi kupewa fedha na timu hiyo ya Jangwani nikaichezee, yeye mwenyewe alikuwa hakijui kisa hicho, nilimuadithia mwenyewe, wakati huo yeye alikuwa anapiga gitaa katika bendi ya Vijana Jazz,'' alisema Gumbo.
Alidai kuwa ukweli wa stori hiyo anaijua Kitwana Manara na Hassan Manento, na kwamba yeye ni Simba damu na hakuna mtu ambaye hajui hilo na ukimwambia mtu kuwa Gumbo ni Yanga haiwezi kuingia akilini.
Wakati huo huo; mjumbe wa kamati ya usajili ya Simba, Mulamu Ng'hambi amepinga vikali taarifa zilizozagaa kuwa yeye ni katibu wa kuajiriwa Simba, amesema wala hajawai kuomba kazi na hafikirii kuomba ukatibu wa kuajiriwa Simba kwa vile klabu hiyo haina fedha za kumlipa.
Alisema yeye ni mwanachama wa Simba na ni friends of Simba ambao lengo la kundi hilo siku zote ni kusaidia maendeleo ya klabu hiyo.
No comments:
Post a Comment