.

.

.

.

Tuesday, August 04, 2009

BENKI KUU YAONYWA


Na Ramadhan Semtawa

SERIKALI imeonya Benki Kuu (BoT), isithubutu kutoa kiasi cha fedha takriban Sh 60 bilioni kwa mfanyabiashara Devram Valambhia, nje ya mahakama.
Onyo la serikali kwa BoT limekuja wakati kumekuwa na shinikizo la Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, kutaka BoT imalize kesi hiyo ya Valambhia nje ya mahakama kwani tayari imetumia kiasi cha Sh 8 bilioni za uwakili hadi mwaka jana Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), alivyofanya ukaguzi.
Wakati kamati hiyo inayoongozwa na mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe, ikitoa msimamo huo kurejea ule wa Kamati ya Fedha na Uchumi, Gavana wa BoT Profesa Benno Ndulu, ametoa msimamo akisema tayari wamepata maelekezo ya serikali yakionya benki hiyo isitoe fedha zake kwa Valambhia nje ya mahakama.
"CAG alionesha wasiwasi kuwa pesa ambazo wakili alilipwa zilikuwa ni nyingi mno kulingana na kesi yenyewe. Kesi yenyewe inagharimu Dola za Marekani 55 milioni na mpaka ukaguzi unafanyika wakili alikuwa amelipwa Sh 8 bilioni," ilisema kamati ikisisitiza umuhimu wa kesi hiyo kumalizwa nje ya mahakama.
Valambhia anaidai serikali kiasi cha dola 55 milioni kutokana na kuiuzia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, magari kutoka Chekoslovakia.
Hata hivyo, akizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalumu ofisini kwake jijini Dar es Salaam wiki iliyopita, gavana Ndulu alisema tayari wamepata maelekezo hayo ya serikali ikionya fedha zake zisiguswe.
"Serikali yenyewe ambayo ndiyo yenye fedha zake, imekataa tusilipe nje ya mahakama..., kwa hiyo ndiyo msimamo uliopo sasa tunaoutekeleza," alifafanua gavana. Gavana alisema BoT siyo yenye dhamana ya kulipa fedha za Valambhia, kwani yenyewe inahifadhi fedha za watu ambazo ni za serikali.
Akifafanua, gavana alisema kama serikali ikitoa idhini BoT haitakuwa na pingamizi, lakini hadi sasa haiwezi na wala haina mpango wa kulipa fedha hizo nje ya mahakama.
"Mwenye pesa kakuonya usiguse fedha zake halafu mwingine aje akwambie uzichukue ukamlipe mtu, hapana... hatwendi hivyo," alisisitiza. Kwa msisitizo, alisema anafahamu lipo shinikizo kutoka kwa watu mbalimbali ambao (ukiacha Kamati ya Bunge), wana maslahi yao.
"Najua kuna watu wanashinikiza hili kwa maslahi yao binafsi, tunawajua, lakini msimamo ni kwamba, I can't do that (siwezi kufanya hivyo)," alisisitiza gavana.
Kamati hiyo ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma katika taarifa yake ya kwanza mwaka huu, imeitaka BoT kumaliza kesi hiyo nje ya mahakama ili kuepuka gharama zaidi za uendeshaji kesi kwa kulipa mawakili.
Hata hivyo, BoT iliijulisha kamati kuwa ilisitisha mkataba na Kampuni ya Mkono tarehe 22 Januari mwaka 2008 na kuteua kampuni nyingine ya Uwakili ya Law Associates, kuitetea BoT katika kesi zake zote.
Sehemu ya taarifa ya kamati ilisema, "Kamati ilifuatilia agizo la Kamati ya Fedha na Uchumi ililolitoa kwa Benki Kuu mwaka 2007 kuhusiana na malipo makubwa ya ada kwa kampuni ya uwakili ya Mkono and Company Advocates. Malipo haya yalitokana na kesi iliyokuwa na inayoendelea mahakamani kati ya Benki Kuu na ndugu Devram Valambhia."
"Kesi hii ni ya siku nyingi sana na inatokana na uamuzi wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa kununua magari kutoka nchini Chekoslovakia."
"Kamati iliona kuwa ni vema kesi hii ikamalizwa nje ya mahakama kwani iwapo itachukua muda mrefu zaidi gharama za kesi zitazidi thamani ya kesi yenyewe. Kamati ya Fedha na Uchumi iliiagiza Benki Kuu kufanya mazungumzo na kampuni ya Mkono ili kupunguza gharama za kesi na hatimaye kuimaliza kesi hiyo nje ya mahakama.
Hata hivyo, kamati ilifafanua kwamba inakubaliana na uamuzi wa BoT kusitisha mkataba na kampuni ya uwakili ya Mkono, lakini ikasisitiza iwapo juhudi hazitawekwa kumaliza kesi hiyo ya Valambhia nje ya mahakama, kampuni ya uwakilii iliyopewa kazi hiyo nayo italipwa fedha nyingi na kwenda zake na ikawa ni mtindo wa mawakili kufaidika na kesi za BoT ambazo haziishi.

No comments:

Post a Comment