.

.

.

.

Saturday, August 29, 2009

FREEMAN MBOWE KUNUSULIWA NA ZITTO KABWE

KATIKA kile kinachoelezwa kuwa ni kunusuru mustakabali wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wazee wa chama hicho leo wanakutana, huku taarifa zikieleza kuwa Zitto Kabwe, ambaye ametangaza kumvaa Freeman Mbowe katika kinyang'anyiro cha Uenyekiti Taifa, anaandaliwa nafasi ya ukatibu mkuu kunusuru mpasuko ndani ya chama hicho.
Mkutano huo unaowahusisha waasisi wa Chadema, akiwamo wenyekiti waliopita, Edwin Mtei na Bob Makani pamoja na wazee wengine kadhaa, unafanyika katika kipindi ambacho tayari wadadisi wa masuala ya siasa wameonyesha wasiwasi wa chama hicho kupasuka iwapo hakutakuwa na busara ya kufanya maamuzi sahihi katika mchakato huo wa uchaguzi.
Iwapo ajenda hiyo ya kumpa Zitto nafasi ya katibu mkuu, itajadiliwa na kupitishwa leo, moja kwa moja itakuwa ni kwa ajili ya kumnusuru Mbowe na chama katika hatari ya kugawanyika. Juzi wazee hao, kwa nyakati tofauti, waliliambia gazeti hili kwamba, uamuzi wa Zitto kugombea ni ukuaji wa demokrasia ndani ya chama hicho.
Mzee Mtei alisema "ndiyo maana kinaitwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo", huku mzee Makani akisema "hakuna mpasuko kwani ni lazima kutakuwa na watu wanaomuunga mkono Zitto na Mbowe, hivyo huo si mpasuko".
Lakini Mwananchi ilipata habari jana jioni zikisema katika kupiga hatua moja mbele kunusuru chama hicho, wazee hao wamepata wazo jipya ambalo ni kufikiria namna bora ya kumtuliza Zitto kwa kumpatia nafasi hiyo ya mtendaji mkuu wa chama ambayo sasa inashikiliwa na Dk Willibrod Slaa, mmoja wa viongozi shupavu ambao wanaheshimika sana katika chama hicho kiutendaji.
Hata hivyo, bado swali linabaki kwamba iwapo Zitto atapewa nafasi hiyo, Dk Slaa atakuwa na nafasi gani kwenye chama hicho.
Tangu kuanza kwa maandalizi ya uchaguzi, Dk Slaa alishawishiwa na wanachama agombee nafasi ya makamu mwenyekiti, lakini alikataa kwa madai anataka kupumzika kazi za chama.
Hata hivyo, wachunguzi wa masuala ya uongozi ndani ya chama hicho wanasema kuwa kuna kundi la wanachama ambao wanataka Dk Slaa agombee urais 2010, lakini mara kadhaa yeye amekuwa akidai hataki nafasi hiyo na kwamba ataendelea kuwatumikia watu wa Karatu kwa nafasi ya ubunge.
Kwa upande wa Mbowe, hali inaonyesha kwamba safari hii hatagombea urais na badala yake ataenda Hai kwa ajili ya kugombea ubunge.
Ingawa watu wengi wanadhani Zitto amekurupuka kugombea nafasi hiyo, lakini watu ambao walio karibu na mwanasiasa huyo wanadai kuwa amejenga mtandao mkubwa kwa muda mrefu ambao utamsaidia sana kupambana na Mbowe.
"Zitto ameshiriki sana kuweka vijana hasa mikoani na Mbowe anakubalika na watu wa mjini na hasa Dar es Salaam na Kilimanjaro, lakini Zitto amejijenga," alisema mmoja wa watu walio karibu na Zitto, 33.
Mapema jana kabla ya taarifa hizo mpya, Zitto, akiwa jijini Dar es Salaam, alisema atakuwa tayari kupokea ushauri wowote utakaotolewa na wazee wa chama hicho.
Alifafanua kuwa huu ni wakati wa uchaguzi, lakini baada ya hapo Chadema itapaswa kuwa chama kimoja kisichokuwa na kambi yoyote.
Zitto alisema kwa mantiki hiyo iwapo atashinda, bado atapaswa kushirikiana na Mbowe na akishindwa, Mbowe atapaswa kushirikiana naye (Zitto), hivyo wanaoeneza propaganda chafu, hawajui nini chama hicho kinapaswa kutendewa.
Zitto, ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Kaskazini, pia alionyesha kuchukizwa na kile kinachoelezwa kwamba anatumiwa na mafisadi na kuhoji: "Ni akina nani hao wanaonitumia... wananitumia ili iweje?"
"Mimi Chadema ni basi langu ambalo nasafiria au sawa na mtumbwi wangu baharini, sasa nitawezaje kuivuruga, halafu nitapata faida gani au nitakwenda wapi,"alihoji.
Alisema kamwe hawezi kutumiwa na mtu yeyote kuvuruga chama hicho kwani ndilo tegemeo la Watanzania kama chama mbadala cha kushika dola.
Zitto hakusita kuweka bayana kwamba Chadema pia ina safari ndefu ya kuunganisha vyama vya upinzani na kujenga umoja imara ambao utakuwa na lengo moja tu la kuleta mageuzi.
"Ukweli ni kwamba NCCR, CUF, TLP na vyama vingine vya upinzani vinatuhitaji na sisi lazima tunavihitaji kushirikiana navyo kwenye maeneo mengi, sasa nitawezaje kuua Chadema badala ya kuimarisha na kuunganisha na wengine," alihoji.
Zitto, mwenye umri wa miaka 33 na mmoja wa wabunge ambao wamekuwa wapambanaji wakubwa ndani ya Bunge, alisema yeye bado mwanasiasa kijana kuliko wote kwenye nafasi ya juu ya uongozi wa Chadema, hivyo haiingii akilini kwamba ataweza kuvuruga chama wakati bado ana malengo ya baadaye kisiasa.
Aliongeza kusema: "Kwa sasa wakati tunajipanga kuelekea katika uchaguzi, mimi nadhani inatupasa tuangalie zaidi maslahi ya chama. Bado kuna maisha baada ya uchaguzi, isije kuwa baada ya uchaguzi tukashindwa kuangaliana. Kama nikishinda nitakuwa katika nafasi nzuri ya kumpigia kampeni Mbowe huko Hai nikiwa kama mwenyekiti wake katika uchaguzi mkuu ujao," alisema Zitto.
Zitto alifafanua kwamba alilazimika kujaza fomu za kugombea kiti hicho akiwa Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere baada ya kushauriwa sana na wenyeviti mbalimbali wa mikoa wa chama hicho.
"Kuna watu wanasema nilijaza fomu kwa mtindo wa kakakuona, lakini inatakiwa wajue kuwa siasa ni staili. Mimi binafsi sikutaka kugombea uenyekiti, lakini shinikizo la wanachama ndilo lililo lilinifanya nigombee, nilijaza fomu nikiwa uwanja wa ndege wakati nikielekea Ujerumani baada ya kuona siwezi kuendelea kuyakataa maombi ya wanachama," alisema Zitto.
"Mimi sina ugomvi wowote na Mbowe labda yeye lakini, kesho wazee wa chama chetu tutakutana nao ili kuangalia kama kuna tofauti zozote tuzimalize," alisema Zitto.
Zitto alisema ana uwezo wa kukiendesha chama kutokana na kuwa na uzoefu mkubwa katika siasa za kitaifa na kimataifa.
"Mimi nimekuwa mshauri wa rais wa Ujerumani kuhusu mambo ya kiuchumi wa bara la Afrika kuanzia mwaka 2006, ni mwenyekiti wa kamati ya bunge ya hesabu za serikali yenye mashirika zaidi ya 193 na thamani ya zaidi ya Sh 3 trilioni, nitashidwa kuiongoza Chadema," alihoji Zitto.
Hata hivyo, alisema kama atashinda na kukishika kiti hicho mwenyekiti wa sasa, wa chama hicho Mbowe atakuwa mjumbe wa halmashauri kuu ya chama hicho kama katiba yao inavyosema.
Naye Mbowe alisema propaganda dhidi ya chama hicho haziwezi kukiyumbisha.
Mbowe, ambaye atagombea nafasi kwa mara ya pili, alisema chama hicho kimetoka mbali na kimejengeka katika misingi ya kidemokrasia, hivyo kila jambo linafanywa kwa uwazi na kwa kufuata kanuni na taratibu za chama hicho.
Mbowe aliliambia gazeti hili jana kuwa mamluki hawakosekani katika taasisi yoyote ile na kusisitiza kuwa maamuzi yote yanafanywa na vikao ndani ya chama na hakuna hata kikao ambacho kimeshakaa hadi hivi sasa.
"Propaganda kutoka kwa watu wa nje na hata baadhi ya vyombo vya habari haziwezi kuvuruga chama chetu, ni wazi kuwa mamluki hawakosekani katika taasisi yoyote ile, lakini chama chetu kina utaratibu wa kuamua mambo yake kupitia vikao mbalimbali. Hakuna maamuzi yanayotolewa bila kuafikiwa na vikao," alisema Mbowe.
Mbowe alisisitiza kuwa uamuzi wa Zitto ni matokeo ya demokrasia ndani ya chama na kuongeza kuwa ana imani kuwa chama kitapita katika kipindi ambacho ni kigumu katika siasa za demokrasia.
"Nina imani tutavuka salama; ni vema Watanzania wakaangalia chama si kwa utashi wa mtu anayeongoza bali kwa kile wananchi wanachofanyiwa na chama. Hiki ni chama cha Watanzania na tuna imani tutavuka salama," aliongeza Mbowe.
Aliongeza hata baada ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mapema mwezi ujao, hatarajii kuwa kutakuwa na chuki na kutoelewana kwa viongozi wa chama hicho kwani wote wanafanya kazi kwa kujitolea na hakuna mshahara wanaolipwa.
"Viongozi wote wa ngazi za juu wanafanya kazi kwa kujitolea, tunachotafuta ni kazi ya kujitolea kuwatumikia wananchi na hakuna 'ulaji'…hakuna anayelipwa mshahara," alifafanua Mbowe.
Mwananchi ilipotaka kujua kama atagombea urais kwa tiketi ya Chadema iwapo atabaki kuwa mwenyekiti wa chama hicho, Mbowe alisema: "Nafasi ya kugombea urais si wajibu wa kudumu wa mwenyekiti. Ni chama ndicho kitakachopendekeza nani na kwa sifa zipi ndio anafaa kugombea nafasi hiyo, alisema.
Mkutano mkuu wa Chadema umepangwa kufanyika Septembe 3 na 4 ambapo utatanguliwa na mkutano wa kamati kuu Septemba 30, na mkutano mkuu wa kwanza wa baraza la wazee utafanyika Septemba 31 mwaka huu.
Mwisho.
Hata hivyo, hadi sasa chama hicho kipo kwenye kipindi cha kigumu cha mpito kuelekea kwenye uchaguzi huo ambao ni mtihaani wa pili baada ya ule wa kifo cha Makamu Mwenyekiti Chacha Wangwe.

Habari hii imeandaliwa na Ramadhan Semtawa, Claud Mshana na Fred Azzah

No comments:

Post a Comment