MAKAZI ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Ikulu ya Rais Jakaya Kikwete, yatakumbwa na giza kwa muda wa siku tano mfululizo, kutokana na kuharibika kwa transfoma kubwa ya vituo vya Masaki na Oysterbay, inayosambaza umeme katika maeneo hayo nyeti.
Maeneo hayo yatakuwa gizani kuanzia Agosti 22 hadi Agosti 26, ambapo kutakuwa na matengenezo makubwa katika transfoma ya kituo cha Masaki.
Taarifa iliyotolewa jana na Meneja Mawasiliano wa Shirika la Umeme nchini TANESCO, Badra Masoud, ilisema kuwa maeneo hayo yatakosa umeme, kwani matengenezo yake yatalazimisha kufumuliwa kwa transfoma nzima na haiwezi kuwashwa tena baada ya kazi hadi itakapotengemaa.
“Ubovu wa vituo hivyo vya transfoma, utasababisha maeneo hayo kukosa umeme kwa muda wa siku tano kutokana na matengenezo makubwa yatakayoanza Agosti 13 hadi 17, mwaka huu katika kituo cha Oysterbay na Agosti 22 hadi 26 katika kituo cha Masaki.
“Matengenezo yatafanyika usiku na mchana ili kukamilisha shughuli hiyo kwa muda uliopangwa, hivyo kuepusha usumbufu wa ziada kwa wateja,” alisema Badra katika taarifa hiyo.
Alisema shirika linalazimika kuifanya kazi hiyo sasa, kwa sababu ya usumbufu mkubwa ambao wateja wa maeneo haya wamekuwa wakiupata kutokana na ubovu huo.
Hata hivyo aliwahakikishia wateja wa maeneo hayo kuwa baada ya matengenezo watapata huduma bora ya umeme.
Mbali na Ikulu na makazi ya Waziri Mkuu, taarifa hiyo iliyataja maeneo mengine yatakayokumbwa na kadhia hiyo kuwa ni ofisi za Ubalozi wa Afrika Kusini na Nigeria, Shule ya Kimataifa ya Tanganyika na baadhi ya nyumba za mawaziri zilizoko eneo la Masaki.
Maeneo mengine ni baadhi ya hoteli za kitalii kama Slipway, Sea Cliff, Golden Tulip, Coco Beach, Coral Beach Club, Yatch Club, Hoteli Karibu, Oysterbay Hotel, Msasani Peninsular na TPDF Masaki.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, maeneo mengine ni pamoja na Barabara ya Kenyatta, Barabara ya Tumbawe, Barabara ya Hill, Mtaa wa Kajificheni, josho la mbwa, nyumba za bandari, Kahama Mining, Toure Drive, Barabara ya Haile Selasie, Barabara ya Chole na eneo la Kanisa la St Peter, vijiji vya Onella, Valhalla, Morogoro Store na Baobao.
Kuhusu maeneo yatakayoathirika kutokana na kuharibika kwa transfoma ya kituo cha Oysterbay yatakayokosa umeme kuanzia Agosti 13 hadi Agosti 17 mwaka huu, taarifa hiyo iliyataja kuwa ni Kinondoni Hananasifu, Moscow, Mkwajuni, Mwananyamala, Ada Estate, nyumba za TANESCO, Drive Inn, Victoria na maeneo ya jirani, Uporoto, Namanga, Msasani Magunia, Barabara ya Kimweri, Karume, Mwananyamala kwa Kopa na Kwale, pamoja na maeneo yanayozunguka mnara mkuu wa Vodacom na Barabara ya Ali bin Said.
Mengine ni Polisi Oysterbay, Barabara ya Laibon, Chunyu, Kenyatta, balozi za Japan, Urusi, India, Kenya na Ufaransa, Barabara ya Kinondoni, ikiwamo Stanbic Bank, Barabara ya Kaunda, Hospitali ya CCBRT na maeneo ya jirani.
No comments:
Post a Comment