.

.

.

.

Monday, October 26, 2009

UMEME WA IPTL GHALI KULIKO DOWANS

• Total waleta shehena ya mafuta tani 7,500

• Yataumika kfua umeme megawati 100

• IPTL kutumia Shs milioni 766 kila siku ya MunguShehena ya kwanza ya mafuta kwa ajili ya mitambo ya kuzalisha umeme ya Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) inawasili leo nchini. Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, alisema Dar es Salaam jana kuwa shehena hiyo itakuwa ni ya ujazo wa tani 7,524. Mitambo ya IPTL itawashwa Jumapili ya Novemba Mosi mwaka huu huku uendeshaji wake ukiigharimu serikali Sh. Bilioni 23 kwa mwezi, sawa na Sh milioni 766 kwa siku. Jumanne wiki hii, Rais Jakaya Kikwete aliagiza kuwashwa mara moja kwa mitambo hiyo inayotumia mafuta baada ya nchi kuingia gizani kutokana na kuharibika kwa mitambo ya Songas na Kihansi. Rais aliziagiza Wizara za Fedha na Uchumi , Nishati na Madini, Katiba na Sheria na Shirika la Umeme (Tanseco) kufanya kazi kila moja kwa nafasi yake kuhakikisha mitambo inawashwa. “Hadi jana (juzi) mchakato wa kupatikana mafuta ulikuwa umekamilika. Wizara ya Fedha na Uchumi imeshajipanga kwa ajili ya malipo ya mzigo huo ili kusiwe na mgogoro wowote.” alisema Ngeleja. Alisema kampuni ya Total Tanzania Limited ndiyo iliyopewa dhamana ya kuleta shehena hiyo. “Ile mitambo inawashwa kwa kufuata taratibu maalum na sasa wataalamu wanaendelea na kikao kati ya Tanesco, mfilisi (RITA), Wartsila, benki ya Standard Chartered, wakijadili gharama mbalimbali kama mafuta na kujua zitumie siku ngapi kuipasha moto mitambo.” alisema. Waziri huyo wa Nishati na Madini aliuhakikishia umma kuwa mchakato wa takwimu zote zinazohusu mitambo ya IPTL kuiwezesha inawashwa zimeshwapelekwa tangu jana Wizara ya Fedha na Uchumi kwa ajili ya uhakiki ili fedha iweze kutolewa. Mtambo wa Songas wenye kuzalisha megawati 20 ulitarajiwa kuwashwa jana , huku mtambo wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) wa Hale – Tanga nao ukiwa umeanza kuzalisha umeme wa megawati kati ya 5 na 6 kutokana na kina cha maji ktotosheleza uwezo wa megawati 8. Awali, Kaimu Meneja Uendeshaji wa kampuni ya Wartsila, Gilbert Ndesamburo, aliwaambia waandishi akiwa pamoja na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja kuwa mitambo hiyo, amabyo illingizwa miaka miwili iliyopita, ikiwashwa kwa saa 24 hutumia mafuta lita 625,000 huku lita moja ya mafuta hayo ikiuzwa kwa Sh 1,200. Ndesamburo alisema kituo hicho kina uwezo wa kuhifadhi mafuta kwa wastani wa tani 15,000 sawa na zaidi ya lita milioni 15. Mitambo hiyo, ambayo ipo kumi na yenye uwezo wa kila moja kutoa megawati 10, ilifungwa nchini mwaka 1998 na ikiwashwa hufua megawati 100 za umeme. Serikali ilikuwa imeagiza mitambo hiyo ibadilishwe iwe inatumia gesi asilia kuiendesha , ili kupunguza gharama za uzalishaji, lakini Wizara ya Nishati na Madini ikasimamisha mchakato huo kusubiri kumalizika kwa kesi ya msingi inayoendelea mahakamani. Katikati ya mwaka huu Rais Kikwete aliagiza mchakato huo wa kubadili mitambo uendelee badala ya kusubiri kesi hiyo kumalizika. Uendeshaji wa mitambo ya IPTL kwa sasa unasimamiwa na kuendeshwa na kampuni kandarasi ya Wartsila,ambayo iliingia mkataba wa miaka miwili na serikali, kuendesha mitambo ya kuzalisha umeme. Mwaka 2006 nchi illingia gizani wakati kulipotokea ukame mkubwa na kusababisha serikali kutafuta suluhisho la haraka ambalo lilisababisha ijikute ikiangukia kwenye kashfa ya Richmond. Kiwango kinachotumiwa na IPTL kufua umeme, kinaanza kufungua sura mpya yenye kuonyesha kuwa kazi ya kuzalisha umeme si lelemama inahitaji fedha nyingi ajabu. Itakumbukwa kuwa Kamati ya Bunge ya Kuchunguza Mkataba Tata wa Richmond, ilisema kuwa serikali ilikuwa inaingia gharama kubwa kulipa Sh. Milioni 152 kwa siku kwa ajili ya kuzalisha megawati 125 kupitia Kampuni ya Dowans. Kwa sasa IPTL watalipwa Sh milioni 766 kila siku ya Mungu kama gharama za uendeshaji na watazalisha megawati 100, ikilinganishwa na 125 za Dowans ambazo zingezalishwa kwa h milioni 152 kwa siku. Kampuni ya Songas ambayo inazalisha umeme megawati 180 hupokea Sh milioni 284 kila siku iendayo kwa Mungu tangu ilipoingia mkataba na serikali. Hii inathibitisha kuwa gharama za kuzalisha umeme ziko juu sehemu zote duniani. Tangu Septemba, mwaka huu, nchi iliingia gizani baada ya kuwepo upungufu wa megawati 180 kwenye gridi ya taifa kutokana na kuharibika kwa mitambo ya Hale na Kidatu. Kwa sasa imeelezwa imetengamaa.

No comments:

Post a Comment