Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo na Demokrasia CHADEMA Freeman Mbowe amekanusha uvumi kuwa yeye na Naibu Katibu Mkuu wake Zitto Kabwe wana 'bifu' na hivyo hawaelewani, huku akitaka taarifa hizo zipuuzwe kwa vile hazina ukweli wowote.
Aidha, Mbowe amekanusha pia madai kuwa CHADEMA kina nia ya kumtimua Zitto na badala yake amesema kuwa Mbunge huyo wa Jimbo la Kigoma Kaskazini (Zitto) ni tegemeo katika chama na kamwe hakuna mpango wowote wa kumuengua.
“Nani anasema mimi nina ugomvi na Mheshimiwa Zitto... sina ugomvi wowote na Zitto. Yeye namchukulia kama kiongozi mwenzangu na mtu muhimu katika chama chetu,” amesema Mbowe.
Akaongeza kuwa CHADEMA kina kazi ngumu mbele ya kuendelea kujiimarisha na hakina muda wa kuanza kuendeleza ugomvi ambao haukijengi chama ila kukidhoofisha.
Akasema kama ni tofauti zilizokuwa wakati wa uchaguzi mkuu wa chama chao, hizo nd'o hazina nafasi kabisa ya kuwagawa kwani zilishamalizwa katika mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika miezi michache iliyopita Jijini Dar.
"Sisi kama viongozi, tulishikana mikono ili kumaliza tofauti zozote zilizokuwapo wakati wa uchaguzi,” akasema Mbowe.
Akizungumzia tuhuma zilizotolewa na viongozi walioondolewa katika nafasi zao hivi karibuni kuwa yeye kama mwenyekiti amekuwa akifuja ruzuku ya chama, akasema hawezi hata siku moja kula ruzuku hiyo, ambayo ni ndogo sana ukilinganisha na mahitaji halisi ya chama.
Akaongeza kuwa hivi sasa, chama chao kinaambulia kiasi cha shilingi milioni 60 kiwango ambacho ni kidogo sana ukilinganisha na majukumu makubwa yanayokikabili chama hicho kitaifa.
"Mimi kama Mwenyekiti silipwi mshahara wala posho na chama ... na wala sitaki kulipwa kwa sababu najua kazi kubwa iliyopo ni kukijenga zaidi chama,” amesema Mbowe.
Aidha, akasema kwa mujibu wa utaratibu, hakuna kiongozi hata mmoja anayeweza kuchukua fedha katika akaunti ya chama bila hicho bila wajumbe wengine kuhusishwa.
"Kwa utaratbu wetu, wanaotia saini ya kuchukua fedha katika akaunti ya chama ni mwenyikiti, katibu na Mkurugenzi wa fedha wa chama... sasa ni wapi ambapo mimi naweza kuchukua fedha za chama peke yangu... hakuna kitu kama hicho!" Akasema.
Kuhusiana na waliofukuzwa uongozi hivi karibuni, Mbowe amesema ni vyema watu wakaelewa kuwa waliondolewa si kisiasa bali kutokana na utendaji wao na siku zote walipaswa kuwajibika kwa katibu mkuu, kwa mujibu wa utaratibu wa CHADEMA.
“Mimi kama mwenyekiti wa chama, huwezi kunifananisha na hao waliofukuzwa kwa sababu mimi sikuteuliwa bali nimechaguliwa, tena na wajumbe wa mkutano mkuu,” amesema Mbowe.
CHANZO: ALASIRI
No comments:
Post a Comment