Na Jackson Odoyo
MADAKTARI wa wilaya ya Temeke wameibua hisia nzito, hofu, simanzi na maswali baada ya kudaiwa kuruhusu mazishi ya watoto wawili mapacha na mmoja wao kuzinduka muda mfupi kabla ya kuingizwa kaburini.
Mtoto huyo, ambaye hadi anataka kuzikwa alikuwa na umri wa siku moja, alishangaza wazikaji baada ya kuonyesha dalili za uhai wakati akiandaliwa kuwekwa kaburini.
Alikuwa bado anapumua na baadaye akaonyesha kufungua macho, kitendo kilichostua wazikaji na kuamua kumkimbiza Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Watoto hao mapacha ni walizaliwa na mama aitwaye Aisha Jabir, 32, mkazi wa Mbagala Maji Matitu ambaye alipelekwa hospitalini hapo Jumamosi kwa ajili ya matibabu.
Baadaye mama huyo alilazwa na saa 11:00 alfajiri ya jana alijifungua mapacha hao, na inadaiwa kuwa madaktari walisema watoto hao walifia tumboni mwa mama yao kabla ya kuzaliwa.
"Baada ya kupata maelezo kutoka kwa watalaam wa afya, tulianza kushughulikia taratibu za mazishi na ilipowadiwa saa 3:00 asubuhi, tukaenda chumba cha mochwari na kuchukuwa miili ya watoto na kuelekea Charambe kwa mazishi," alisema mtoa taarifa wa Mwananchi.
"Ndugu yangu!!! katika maisha yangu sijawi kukutana na tukio la aina hii, tulichimba kaburi moja kwa ajili mazishi yao na tukiwa makaburini tukaanza shughuli za mazishi na baada ya kumweka mtoto mmoja kaburini, tukamfunua wa pili ili tumvishe sanda, kabla ya kumweka shimoni ndipo tukabaini kuwa yu hai." Alisema mtoto huyo alipofunuliwa alionekana anapumua na baada ya kupigwa mwanga wa jua akafumbua macho.
"Siwezi kusema kilichotea baada ya hapo, isipokuwa tulimkimbiza Hospitali ya Temeke kwa matibabu zaidi huku mmoja ambaye alishafariki dunia akazikwa," alisema. Baada ya kufikishwa Temeke, madaktari waliamua apelekwe Muhimbili kwa matibabu zaidi.
Mganga mkuu wa Hospitali ya Temeke, Aisha Mahita alisema hakuwa na taarifa yoyote kuhusu tukio hilo, lakini akaahidi kufuatilia habari hizo afahamu undani wake.
"Kwanza, nashukuru kwa taarifa pili naomba unipe muda ili nifuatile undani wa suala hilo ili nikupe jibu sahihi," alisema Dk Mahita.
Habari zinasema kuwa mama huyo alipelekwa hospitalini hapo akiwa na ujauzito wa miezi saba baada ya kupata matatizo ya afya kwa zaidi ya siku mbili.
Baada ya kupimwa, alionekana ana ujauzito wa watoto mapacha. Baba wa watoto hao, Ally Athuman Mnimesa, 36, alisema:
"Baada ya kufika hospitalini, mgonjwa alilazwa lakini cha kushangaza wauguzi wakaniambia nilipe Sh 3,000 kwa ajili huduma ya kujifungua. Nikawauliza kwani amekuja kujifungua, wakasema huo ni utaratibu wao," alisema Mnimesa.
"Saa 11 alfajiri, walinipigia simu kuwa mke wangu amejifungua mapacha wawili, lakini wote imekuwa bahati mbaya, hivyo inatakiwa nitoe Sh15,000 ili mama yao asafishwe kizazi."
Baba huyo alisema suala hilo linamuumiza akili kiasi kwamba hawezi kuendelea kulizungumzia zaidi isipokuwa msemaji wa familia.
Mama wa mapacha hao alisema kuwa hali yake bado haijaimarika lakini amepata taarifa kuwa mtoto wake anaendelea vizuri baada ya kupata matibabu. Lakini, kutokana na hali yake baadaye alishindwa kuendelea na mahojiano huku akilalamikia maumivi makali ya mgongo.
"Mwanangu nimeambiwa anaendelea vizuri isipokuwa mimi hali yangu bado si nzuri kwa sababu ninasikia maumivu makali sana, kuanzia kiunoni hadi mgongoni," alisema Jabir.
No comments:
Post a Comment