.

.

.

.

Monday, January 18, 2010

RAIS KARUME NA SEIF SHARRIF HAMADI KUTOYUMBISHWA

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad ameibuka na jambo jipya baada ya kudai kuna ‘kundi la wanga’ wanaotaka kukwamisha makubaliano waliyoafikiana yeye na Rais Aman Abeid Karume kwa ajili ya kuongezewa muda wa kuendelea kutawala kisiwani humo.
Maalim Seif alitoa kauli hiyo, alipowahutubia wafuasi wa chama hicho, katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Kibandamaiti mjini Zanzibar.
Hata hivyo, alisema ‘kundi la watu wanga’ halitafanikisha azma yake, kwa vile yeye na Rais Karume Novemba 5 mwaka jana, walikubaliana kwa dhati kuwaunganisha Wazanzibar ili kuzaa Zanzibar mpya itakayokuwa na misingi mizuri ya demokrasia na uchumi wake.
Alisema kwa msingi huo, ndio maana CUF imeamua Rais Karume aongezewe muda ili akamilishe kazi aliyoianzisha kwa vile kama ataondoka kabla ya kukamilisha kazi hiyo, watu walioyapokea kwa kinyongo maridhiano hayo watafanikisha nia yao mbaya.
“Mimi na Rais Karume tumesema haturudi nyuma tena na anayechukia achukie, wengine wamekosa kusema wanahoji leo Seif anampenda Karume,” alisema Maalim Seif.
Maalim Seif, alisema hivi sasa wanga wasiotaka maridhiano wameshaanza kufanya chokochoko kwa kueneza maneno ya uongo huko Tanzania Bara na Zanzibar, eti Rais Karume na Maalim Seif wanataka kuvunja Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Alisema suala la kubadilisha Katiba na kuongezewa muda Rais Karume liko ndani ya maamuzi ya Wazanzibari wenyewe kupitia Baraza la Wawakilishi kwa sababu wao ndio wenye maamuzi ya mwisho.
“Tunazungumzia Katiba ya Zanzibar na utawala wa Zanzibar, wewe kule bara katiba haikuhusu, sie njia yetu moja tu ya kuamua ni Baraza la Wawakilishi,” alisema Maalim Seif.
Alisema suala la kubadilisha Katiba ni jukumu la wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa vile halina uhusiano na CCM au Serikali ya Muungano.
Maalim Seif alisema Rais Karume anayo nafasi kubwa ya kuendelea na CUF inamuomba akubali kwa vile suala la kuahirishwa uchaguzi sio geni kwa sababu mwaka 2005, Serikali ya Muungano iliahirisha uchaguzi kufuatia mgombea mwenza wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kufariki.
“Uchaguzi ucheleweshwe tupate kumlea mtoto, haiwezekani mtoto alelewe na mwanga,” alisema Maalim Seif na kusisitiza watu wanaotaka kumrithi Rais Karume nafasi yake wamekuwa wakitizama kwa jicho baya mustakabali wa maridhiano.
Msimamo wa Hamad umekuja siku chache tangu viongozi wa CCM, akiwemo Makamu Mwenyekiti bara, Pius Msekwa, na Katibu Mwenezi wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, kusema Katiba haitabadilishwa kwa lengo la kumwezesha Rais Karume kuendelea kubakia Ikulu kwa vile muda wake umefikia kikomo.
Akisoma risala ya wananchi wa mikoa mitatu ya Unguja, Katibu wa Wilaya ya Kusini, Mohammed Kombo, alisema wanachama wa chama hicho wanaunga mkono uchaguzi kuahirishwa ili Rais Karume kuongezewa muda.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Juma Duni Haji, alisema wale wote wenye hoja kwamba Katiba haiwezi kubadilishwa kumwezesha Rais Karume kuendelea, anawasubiri katika Baraza la Wawakilishi kwa vile yeye tayari ni mjumbe wa baraza hilo.
Tayari kiongozi wa upinzani katika Baraza la Wawakilishi, Abuubakar Khamis Bakari, anadaiwa kuandaa hoja binafsi ya kutaka kuundwa kwa serikali ya mpito itakayomwezesha Rais Karume kuendelea kubaki madarakani kwa muda wa miaka mitatu.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana kupitia kwa baadhi ya wajumbe wa kampeni kuhusu mpango huo, wameeleza kwamba suala hilo limefikia hatua kubwa kwa vile tayari wajumbe wengi wa CCM wameonekana kushawishika na kuunga mkono hoja hiyo.
Januari 12 mwaka huu wakati wa sherehe ya kutimiza miaka 46 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Rais Karume, aliutangazia umma kuwa hatagombea tena urais kwa vile vipindi vyake viwili vimemalizika kwa mujibu wa Katiba.

No comments:

Post a Comment