.

.

.

.

Wednesday, January 27, 2010

WALIOUWA KUPANDISHWA KIZIMBANI LEO

ASKARI wawili wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), wanaodaiwa kumuua Swetu Fundikira(45), wanatarajiwa kupandishwa kizimbani leo.
Askari hao, ambao ni mtu na mke wake kutoka kambi ya Lugalo, wanadaiwa kumuua kijana huyo, Swetu Fundikira baada ya kumpiga wakiwa na mwanajeshi mwingine mmoja katika ugomvi wa barabarani uliotokana na askari hao kudai kuwa walifanyiwa fujo na kutukanwa na mareheremu Swetu.
Kwa mujibu wa habari kutoka ndani ya Jeshi la Polisi, askari hao, Sajenti Rhoda Robert, ambaye ni askari wa Jeshi la Wananchi kutoka Lugalo, na Koplo Ali Ngumbe ambaye ni mume wa Sajent Rhoda, wanatarajiwa kupandishwa kizimbani leo baada ya taratibu za kuwapandisha kizimbani jana kutokukamilika.
"Watuhumiwa hao walipaswa kupandishwa kizimbani jana, lakini hawakuweza kupandishwa kwa sababu taratibu hazikukamilika ikiwa ni pamoja na maandalizi ya hati ya mashtaka.
"Kwa hiyo, kesho ni lazima watapandishwa kizimbani, ingawa sina uhakika zaidi watashtakiwa katika mahakama gani, lakini ni kati ya Kinondoni na Kisutu. Uwezekano mkubwa ni katika Mahakama ya Wilaya ya Kinodnoni kwa sababau ndiko tukio lilikofanyika," kilisema chanzo chetu cha habari kutoka ndani ya jeshi la Polisi.
Swetu alifariki dunia Jumapili usiku katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kutokana na kipigo cha wanajeshi hao, na watuhumiwa hao walitiwa mbaroni na askari polisi wa kituo cha Salender Bridge, na kupelekwa katika kituo cha polisi Oysterbay.
Habari kutoka kwa watu walioshuhudia tukio hilo, zilisema kuwa askari hao walimpiga kijana huyo juzi katika eneo la Kinondoni A kwa kwa Manyanya madai kuwa aliwachomekea gari lake, na kwamba baada ya kumpiga walimchukua na kumuingiza ndani ya gari lao na kuondoka nalo ambapo waliendelea kumpiga huko njiani.
"Tulidhani wanampeleka hospitalini kumbe walipofika karibu na Hospitali ya Muhimbili walimshusha na kuendelea kumpiga na raia mwema alipowaona alitoa taarifa katika kituo cha Salender Bridge. Askari polisi walifika eneo la tukio na kuwakuta wakiendelea kumpiga ndipo wakawatia mbaroni wanajeshi hao," alisema shuhuda huyo.
Kamanda wa polisi Kinondoni, Elias Kalinga alisema mbali na watuhumiwa hao, , mwanajeshi mwingine aliyefahamika kama Private Mohamed Ngumbe, ambaye pia alikuwa kwenye gari moja na watuhumiwa hao, hajakamatwa na bado anasakwa.
"Askari hao walimpigia honi marehemu wakitaka awapishe, lakini akakataa ndipo walipompiga baada ya kukataa kuwapisha," alisema Kamanda Kalinga.

No comments:

Post a Comment