.

.

.

.

Monday, April 12, 2010

SIMBA NA YANGA KUCHEZA TAIFA USIKU

BAADA ya miaka 18, tangu zilipocheza mechi usiku visiwani Zanzibar, mchezo wa watani wa jadi Yanga na Simba kwa mara ya kwanza katika ardhi ya Tanzania Bara utachezwa usiku saa 2.00 usiku kwenye Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.

Mechi hiyo ya marudiano ya Ligi Kuu itakuwa ni mara ya pili kwa klabu hizo mbili kucheza usiku tangu zilipofanya hivyo Februari 1992 wakati wa fainali ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati katika mchezo uliochezwa katika uwanja wa Amani Zanzibar na Simba kutoka kidedea kwa mikwaju ya penalti kwa 6-5 dhidi ya Yanga.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania ( TFF) Fredrick Mwakalebela alisema kuwa mchezo huu utafanyika kuanzia saa 2.00 usiku na milango itaanza kufunguliwa kuanzia saa 10.00 jioni ilikuwapa fursa ya watu kuingia mapema na kupunguza msongamano.

Alisema lengo la kuweka mechi hiyo usiku ni kwa sababu ya kazi ya kiserikali itayofanyika siku hiyo nje ya uwanja huo na klabu zote zimeridhia mchezo huo uchezwe usiku.

''Siku hiyo itakuwa ni siku ya Maji Duniani kwa hiyo Benki ya Exim imeanzaa mbio fupi kwa ajili ya kuchangia fedha za upatikanaji wa maji Tanzania ambazo zitaanzia nje ya uwanja wa Taifa hivyo kwa kuwa ni kazi ya kiserikali tumeona ni bora tukaipisha kazi hiyo na mechi yetu iwe usiku,'' alisema Mwakalebela.

Pia, aliongeza kuwa kuweka mechi hiyo usiku itakuwa imewarahisishia mashabiki wa pande zote mbili kufanya kazi zao za mchana kutwa na usiku kuja kuzishuhudia timu zao.

Viingilio vya mchezo huo ambapo sasa wapenzi wa soka watakaokaa viti vya VIP A watalipa Sh 40,000, wakati VIP B ni Sh 30,000 na VIP C ikiwa ni Sh 20,000.

Viti vya rangi ya mkabala na magoli ni Sh 15,000 na vile vya rangi ya machungwa nyuma ya magoli ni Sh10,000, viti vya bluu ni Sh 7,000 na viti vya kijani ni Sh 5,000.

Mchezo huu ulipangwa kufanyika jana katika uwanja wa Uhuru baada ya Taifa kwa kile walichodai kukwepa asilimia 20 inayochukuliwa na serikali ikiwa ni gharama za uwanja kabla serikali haijaingilia kati na kutaka maongezi ya klabu hizo mbili kuhusu asilimia hiyo na kupeleka mbele mechi hiyo mpaka Jumapili.

No comments:

Post a Comment