.

.

.

.

Tuesday, May 04, 2010

SIMANZI MKOANI KILIMANJARO

Maziko ya watoto waliouawa na mama yagubikwa na simanzi Na Nakajumo James, Moshi MTAA wa Kariwa Kata ya Rau katika Manispaa ya Moshi jana uligubikwa na simanzi wakati wa maziko ya watoto watatu wa familia moja waliouawa kikatili na mama yao mzazi wiki iliyopita.

Katika maziko hayo yaliyoongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Mussa Samizi, watu kadhaa walizimia baada ya kushuhudia miili ya watoto hao.

Wengine walioshiriki maziko hayo ni Mbunge wa Moshi Mjini, Philemoni Ndessamburo na viongozi wengine wa vyama vya siasa.

Maziko yalifanyika nyumbani kwa wazazi wa watoto hao kwa Ibada iliyoongozwa na Padri wa Kanisa Katoliki, Patrick Asanterabi.

Mama mzazi wa watoto hao, Benedicta Thadei(44) aliwaua wanawe hao Aprili 29 saa 12 asubuhi.

Watoto hao ni Antony Thadey (3), Noela Thadey (5) na Rose Thadey (13) ambaye pia alikuwa na ulemavu wa akili na viungo.

Mtuhumiwa huyo pia alimjeruhi mtoto mwingine, Pascal Thadei (9) ambaye amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC kwa matibabu zaidi huku ikiripotiwa kuwa hali yake ni mbaya.

Akizungumzia tukio hilo, mama mdogo wa baba wa watoto waliouawa, Mary Kazimoto, alisema mwanamke huyo awali hakuwa na ugonjwa wa akili.

Kazimoto alisema mara baada ya maziko hayo, familia inatarajia kufanya kikao cha ukoo ili kujadili suala hilo na kulitafutia ufumbuzi ikiwa ni pamoja na kuangalia mustakabali wa watoto watatu waliobaki.

Wakati mauaji hayo yakifanyika baba wa marehemu hao, Aloyce Thadey hakuwepo nyumbani.

Polisi inamshikilia mtuhumiwa ambaye kwa taarifa za awali, zinadai anapata matibabu ya ugonjwa wa akili katika Hospitali ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi.

No comments:

Post a Comment