.

.

.

.

Monday, September 06, 2010

TANZANIA KUWA YA KWANZA KWA KUVUNA URANIUM DUNIANI

MRADI wa kuchimba madini ya uranium Mkoa wa Ruvuma utakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 1,650 kwa mwaka na hivyo kuifanya Tanzania kuwa kinara wa madini hayo duniani, ilifahamika.

Hatua hiyo hiyo itasababisha kuicha nyuma nchi ya Marekani ambayo kwa sasa inavuna tani 1,560 za madini hayo kwa mwaka na kuwa nchi ya kwanza duniani kwa kazi hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa mradi huo wa Kampuni ya Mantra Resources Ltd Tony Devlin alisema hayo mwishoni mwa wiki mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dk Christine Ishengoma alipozungumza na waandishi wa habari waliotembelea mradi huo.

Delvin alimhakikishia Mkuu wa mkoa kwamba mradi huo ni mkubwa na kwamba kinachohitajika ni ushirikiano baina ya wananchi, kampuni na serikali kwa ujumla ili kufanikisha mradi huo.

Akizungumza machache, Mkuu wa mkoa alisema mradi wa madini ya uranium katika Mto Mkuju wilayani Namtumbo, ni hazina na kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi wa
Tanzania.

Ishengoma alisema mradi huo, utakuwa chachu kubwa katika maendeleo ya wilaya hiyo, mkoa na taifa kwa jumla, kwa sababu utavutia shughuli nyingi za kiuchumi.

"Huu ni mradi wa kujivunia kitaifa kwa sababu utakuwa na manufaa mengi katika jamiii ya watu wa Ruvuma na Tanzania kwa jumla maana utavutia shughuli nyingi za kijamii na kiuchumi," alisema.

Mkuu huyo wa mkoa alisema pamoja na mambo mengine, mradi huo utazalisha
mamia ya ajira kwa vijana na hiyo kupunguza tatizo la ajira miongoni mwa wananchi.

"Tumeambiwa na Meneja wa mradi kuwa mahitaji yao mengi kama chakula watanunua
kutoka ndani ya nchi hivyo wafanyabiashara na wakulima kwa jumla watakuwa na
nafasi nzuri ya kufanya biashara na mradi huo," alisema Ishengoma

Aliwataka wakazi wa Namtumbo na Mkoa wa Ruvuma kwa jumla, kuchangamkia
fursa hiyo adhimu inayotafutwa na watu wa maeneo mengine nchini.

"Lakini pamoja na nafasi hii naomba niwape tahadhari kuwa msidhani kila
mtakachozalisha kitanunuliwa, hapana , kinachotakiwa ni kuzalisha vitu vyenye
ubora unaoendana na hadhi ya mradi husika," alisema.

Alisema uongozi wa mkoa kwa upande wake, utatoa ushirikiano wa
kutosha kwa mradi huo na kuwataka wananchi kujenga
mahusiano mazuri na wawekezaji.
Sisi kama viongozi wa mkoa, tumevutiwa sana na mipango ya
mradi hivyo na kwa hiyo tunaiomba serikali kuu kwa upande wake ,iwape ushirikiano wawekezaji
hawa," alisema Ishengoma.


No comments:

Post a Comment