.

.

.

.

Saturday, December 25, 2010

MATUKIOUK INAWATAKIA KRISMASI NJEMA WADAU WAKE WOTE DUNIANI

Leo ni siku ya Krismasi ambapo Wakristo wote duniani wanaungana kusheherekea kuzaliwa kwa Bwana Yesu Kristo zaidi ya miaka 2000 iliyopita. Ni siku ambayo Biblia Takatifu inasema kuwa mtoto Yesu Kristo alizaliwa katika mji wa Daudi uitwao Bethelehemu katika mazingira magumu na ya kimasikini, ikiwa ni namna ya kuufundisha ulimwengu umuhimu wa kuishi maisha ya uadilifu na unyenyekevu.

Kwa Wakristo, siku hii ni fursa ya kutawanya na kueneza ujumbe wa upendo, amani na upatanifu. Ujumbe wa Krismasi hutoa nanga ya amani kwa wale wenye nia ya kujenga jamii katika misingi ya kiroho na uwajibikaji wa pamoja. Ujumbe wa kipindi cha Krismasi huwakumbusha Wakristo kote duniani umuhimu wa kujirudi na kuacha dhambi na kuwatendea mema binadamu wote.

Biblia Takatifu inasema kuwa chimbuko la ujumbe huo wa kikristo ni upendo wa Mungu aliyewaumba binadamu na wito wake wa siku zote wa kuwahimiza kuwapenda majirani zao kama wanavyojipenda wenyewe. Ni ujumbe rahisi na wenye maana nzito, ingawa Wakristo wengi hudhani kuwa ni mgumu sana kuutekeleza. Ndio maana kila sikukuu ya Krismasi inapowadia, viongozi wa dini ya Kikristo katika madhehebu mbalimbali, huwahimiza tena waumini wao kuonyesha upendo kwa watu wote na wakati wote pasipo kujali tofauti za dini, kabila na jinsi.

Lakini kama mafundisho ya dini zote yanavyotukumbusha mara kwa mara, matatizo mengi yanayozikabili serikali nyingi na watu wengi duniani kamwe yasingekuwapo iwapo kila mtu angemtendea mwenzake kama ambavyo yeye angetaka atendewe. Kuwapo machafuko katika nchi yoyote kwa sababu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kama ilivyo huko Somalia na Ivory Coast au kama ilivyokuwa Rwanda, Burundi, Liberia na Siera Leone ni matokeo ya ubinafsi na ubaguzi ambavyo ni vichochezi vikuu vya vurugu, chuki na vita.

Ni kwa sababu hiyo tunategemea kwamba viongozi wa madhehebu ya Kikristo katika ibada za misa zao leo watatumia fursa hii ya kuadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo kukemea maovu katika jamii yetu ambayo kimsingi ndio vyanzo vya ukosefu wa upendo na uvunjifu wa amani. Kwa mfano, rushwa inaendelea kutafuna misingi ya umoja, amani na mshikamano wa Watanzania kutokana na viongozi wetu kukosa uzalendo na upendo kwa nchi yao na watu wake.

Kwa sababu ya kutaka kutawala milele, watawala wetu wamekosa utashi wa kisiasa wa kuipa nchi yetu katiba mpya itakayokidhi matakwa na matamanio ya wengi ili kutuepusha na uwezekano wa kuwapo vurugu na maangamizi katika taifa letu siku za baadaye. Viongozi wa Kikristo wachukue fursa ya maadhimisho ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo leo kuwaombea watawala wetu wapate ufunuo ili waone umuhimu na wakubali kwa dhati kuanza mkakati wa kuandika katiba mpya haraka iwezekanavyo.

Sisi tunawatakia kila la kheri Wakristo wote na wananchi kwa ujumla katika kusheherekea siku hiyo, na tunatoa rai kwamba katika kufanya hivyo, wachukue tahadhari ili kuepuka maafa, hasa ajali za barabarani ambazo tayari zinachukua maisha ya watu wengi kila kukicha. Ajali nyingi hutokana na shamrashamra za aina nyingi ambapo watu hula na kunywa, lakini kama wasomaji watakavyoona katika makala tuliyoyachapisha katika ukurasa wa tatu wa toleo hili, viongozi kadhaa wa Kikristo wanaonya kuwa kusheherekea kunapaswa kutanguliwa na maana ya kiroho ya kuzaliwa kwa Kristo.

Ni imani yetu kuwa Wakristo watawaelewa viongozi wao hao wa kiroho wanaposema kuwa baadhi ya Wakristo wanapotoka kwa kuacha kusudi la msingi la kuzaliwa kwa Yesu Kristo ambao ni ukombozi na badala yake wanafanya sherehe kubwa za vyakula na vinywaji, na pengine kushiriki katika anasa ambazo kimsingi zinamchukiza Mungu.

1 comment:

 1. Mimi naitwa Ebou Shatry Kutoka Washington DC
  Asante sana kamanda mungu akubariki kwa pongezi zako na kurasa nzima ya kupongeza merry x-mas kwa wote kila la kheri.
  Ila naomba na mimi Uniwekee Blog yangu kwako na kuizindua Rasmii hapo Uk kesho kama itawezikani. jina la blog ni http://swahilivilla.blogspot.com/

  imeanzishwa mjini Washington Dc na inaendeleza kazi zake katika mji wa Maryland. Inatumia lugha ya kiswahili na kingereza ili kuhabarisha kuhusu maswala mbalimbali ya kijamii hasa katika ukanda wa Marekani mashariki na Afrika mashariki. Itakuwa inakuletea habari mbalimbali za kijamii, siasa, burudani,michezo nk. Nakaribisha maoni yenu. Wasiliana nasi kwa. Email:kijiko12@hotmail.com

  Natashukuru ukifanya hivyo tuta saidiana katika kupandisha mlingoti wa habari zaidi. Na unisomapo usisite kuweka neno kwani ni chanzo chakuelewa hali halisi inayokubalika katika jamii yetu kwa jumla. shkran mzee wa uk.

  ReplyDelete