.

.

.

.

Wednesday, March 02, 2011

APORWA MIL.30

WATU wanne wanaosadikiwa kuwa ni majambazi, jana walimvamia mkandarasi wa Kampuni ya Ujenzi ya Heinan International ya China, Hemao Edson (23) na kumpora zaidi ya Sh milioni 30 wakati akitoka benki.

Tukio hilo lililodumu kwa takribani dakika nne, lilitokea saa 5.40 asubuhi eneo la Morocco katika Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam wakati Mchina huyo akiendesha gari lake aina ya Toyota RAV 4 lenye namba za usajili T544 DEU, akitoka kuchukua fedha hizo katika Makao Makuu Benki ya ABC katikati ya Jiji.

Inadaiwa mara baada ya kufika katika eneo hilo la Morocco karibu na taa za kuongozea magari, majambazi hao wakiwa na gari aina ya Toyota Mark II ambayo hata hivyo namba zake hazikuweza kujulikana, walikwenda mbele ya gari la Mchina huyo kisha kumzuia kwa mbele, wakashuka.

Baada ya kushuka, inadaiwa mmoja wao alichukua jiwe kubwa lililokuwamo ndani ya gari lao kisha kuvunja kioo cha gari la Mchina na kumuamuru kutoa fedha alizokuwa amezibeba huku wakimtishia kumuua endapo angekaidi agizo hilo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa hali ya Mchina huyo ni nzuri licha ya kupata michubuko mikononi na kwamba hakuna aliyekamatwa.

Alisema, haikujulikana mara moja majambazi hao walikuwa na aina gani ya silaha wakati wa uhalifu huo, isipokuwa jiwe ndiyo silaha ya kwanza iliyobainika ilitumika kuvunjia kioo cha gari hilo.

No comments:

Post a Comment