Kizitto Noya na Venance George,Loliondo
MCHUNGAJI Ambilikile Mwasapile amesema hivi karibu atahamisha utoaji wa tiba katika eneo analoishi sasa na kwenda sehemu ambayo itakuwa na nafasi kubwa zaidi, kwa lengo la kupanua huduma na kubadilisha mazingira anayoishi.
Akizungumza juzi mchana kijini hapo, mchungaji huyo alisema yeye si mganga wa kienyeji, bali anatibu kwa miujiza ya Mungu na kusisitiza kwamba ili mgonjwa apone anatakiwa kuwa na imani katika huduma hiyo.
"Nataka nieleze kidogo kuwa mimi si mganga wa kienyeji. Tiba yangu ni miujiza ya Mungu ambaye ameamua kuliweka neno lake katika mti huu ili lilete uponyaji.
Ameamua kuukomesha ugonjwa wa Ukimwi duniani kabisa," alisema mchungaji huyo na kuongeza:
“Kwa wale wanaoumwa Ukimwi wanapokunywa dawa hii wanapona kabisa. Tiba itaanza kujidhihirisha ndani ya siku saba. Lakini wadudu hata kama bado watakuwapo, hawatakuwa na nguvu na katika kipindi cha miezi mitatu, wadudu wote watakufa kabisa.
Kwa wale wenye kansa, dawa inamaliza kabisa tatizo hilo, dawa hii inaponya kichaa, kifafa na magonjwa mengine ambayo mgonjwa atataka apone."Idadi ya wagonjwa wanaomiminika kwa Mchungaji Mwasapile inazidi kuongezeka siku hadi siku. Hivi sasa wanakaa foleni kati ya siku tatu na tano kabla ya kupata tiba hiyo.
Wengi wanailalamikia Serikali kwa kushindwa kumsaidia mchungaji huyo kuboresha mazingira ya utendaji kazi wake. Mmoja wa wagonjwa waliokuwa wakisubiri tiba hiyo, Sara Ibrahim alisema: "Huduma ni nzuri lakini hakuna ulinzi wa maana. Hakuna 'ambulance' (gari la wagonjwa), watu wanafia kwenye magari kwa kukosa msaada wa karibu kuwafikisha kwa mchungaji. Tunaiomba Serikali isaidie huduma hiyo pia kwa kujenga vyoo, kusambaza maji na kutoa jenereta."
Licha ya malalamiko hayo, barabara ya kufika huko inazidi kuharibika na kusababisha mamia ya wagonjwa na jamaa zao kukwama porini. Zaidi ya abiria 600 waliokuwa wanatoka Arusha kwenda huko wamekwama umbali wa kilometa 306 kutokana na ubovu huo.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Mwananchi ilishuhudia magari 68 yenye uwezo wa kubeba zaidi ya abiria 10 kila moja, yakiwa ama yamepasuka magurudumu au yamepata pancha katika barabara hiyo iliyojaa mashimo baada ya mvua kubwa kunyesha Jumamosi iliyopita.
Mmoja wa madereva wa magari hayo ya kitalii, Aman Mshanga alieleza moja ya sababu za magari hayo kukwama njiani kuwa, ni pamoja na mengi kutofanyiwa matengenezo kabla ya kuanza safari. Alisema kutokana na umuhimu wa barabara hiyo katika siku za hivi karibuni, Serikali inapaswa kuifanyia matengenezo.
Alisema Barabara ya Arusha kwenda Loliondo, hasa katika Kijiji cha Samunge anakofanyia matibabu mchungaji huyo itaendelea kuwa mbaya kiasi cha kukosa mawasiliano kabisa katika siku za hivi karibuni kama hakutakuwa na jitihada za kuitengeneza.
Hata hivyo, wakati dereva huyo akisema kwamba sababu za magari hayo kukwama njiani ni kutokana na ukosefu wa matengenezo kabla ya safari, polisi mkoani Arusha imekuwa ikieleza kuwa chanzo cha ajali hizo ni mwendokasi wa madereva.
Mmoja wa wagonjwa, Anna Ibrahim alisema: "Kila gari linalofika Samunge linatozwa Sh2,000 lakini barabara bado ni mbovu na hatujui fedha hizo zinakwenda wapi? Serikali inatakiwa itumie kodi yetu kutuletea maendeleo,” alisema. Hadi kufikia juzi, idadi ya magari yanayopeleka wagonjwa kwa Mchungaji Mwasapile yanakadiriwa kufikia 40,000.
Akizungumzia ongezeko hilo la wagonjwa wanaokwenda kwake kupata tiba, Mchungaji Mwasapile alisema hiyo ni sehemu tu ya watu watakaotoka maeneo mbalimbali duniani kuifuata huduma hiyo kwake... "Watu wataendelea kufurika hapa kutoka kila pembe ya dunia na maajabu ya Mungu yataendelea kujionyesha."
SOURCE: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment