Mganga mwingine wa tiba za magonjwa Sugu aliyefahamika kwa jina la Jafar Welino(17) mkazi wa mtaa wa Mianzini Kitongoji cha Mabatini jijini Mbeya ameibuka na kutoa tiba kwa mamia ya wakazi wa jiji la Mbeya na viotongoji vyake.
Umati wa watu ulionekana katika nyumba anayoishi kijana huyo wakisubiri kupatiwa tiba hiyo huku wakiwa na vikombe vyao mikononi.
Baadhi ya wananchi waliofika eneo hilo walidai kuwa wamefika hapo kutokana na taarifa za kuwa kijana huyo anatibu magonjwa Sugu bure kama vile ambavyo anatibu Mchungaji mstaafu wa Loliondo Mzee Ambilikile Mwasapila.
Akizungumza kwa niaba ya kijana huyo mama mkubwa wa mganga huyo aliyejitambulisha kwa jina la Edina Sanga alisema kuwa kijana huyo alianza tiba hiyo wiki mbili zilizopita ambapo kabla ya kuanza kutibu alimueleza mama yake huyo kuwa alitokewa na mama yake mzazi a,mbaye kwa sasa ni marehemu akimuelekeza kurithi mikoba yake.
Bi.Sanga alisema kuwa mama yake kijana huyo ambaye kwa sasa ni marehemu alikuwa ni mtu mwenye maruhani ambapo kwa kutumia maruhani hayo alikuwa akitoa tiba kwa wakazi mbalimbali mjini Mbeya.
Alisema kijana huyo ambaye wamezaliwa mapacha na dada yake aliyemtambulisha kwa jina la Hadija Welino kwamba yeye anasoma kidato cha Nne katika shule ya sekondari Itende.
Hata hivyo Bi.Sanga alisema kuwa kijana huyo aliitwa katika ofisi ya Ofisa Mtendaji ili kutoa maelezo ya namna ambavyo anaendesha tiba hiyo na kuwa hata hivyo anaendelea kutoa tiba kwa watu kwa kunywa vikombe viwili kwa muda wa siku mbili.
Alisema kuwa dawa hiyo aliifuata katika kijiji cha Iyula kilichopo wilayani Mbozi na kuwa mara alipofika alianza kuichemsha na kuwagawia wananchi wanaosumbuliwa na maradhi sugu.
Aidha umati wa watu walikuwa wamejipanga katika mistari kusubiri tiba hiyo ambapo
Mwenyekiti wa mtaa wa Mianzini Bi.Elizabethy Mwakabungu aliweka utaratibu wa wananchi kupata tiba ikiwa ni pamoja na kuchangia fedha kidogo kwa ajili ya kununulia kuni za kuchemshia dawa hiyo.
Akizungumza na umati wa watu waliokuja kujipatia tiba hiyo Mwenyekiti huyo wa mtaa alisema kuwa kila ambaye atapata kikombe kimoja cha dawa anatakiwa kupata kikombe cha pili siku inayofuata.
‘’Mganga katuagiza kuwa kila anayekunywa kikombe kimoja anatakiwa kunywa kikombe cha pili siku inayofuata…yeyote atakayekunywa hatakiwi kunywa pombe kwa muda wa siku saba,’’alisema Bi. Mwakabungu.
No comments:
Post a Comment