.

.

.

.

Wednesday, March 23, 2011

SIMANZI ! SIMANZI! SIMANZI!

VILIO, simanzi na huzuni vimegubika kwa sehemu kubwa jiji la Dar es Salaam kufuatia vifo vya wasanii 13 wa muziki wa taarabu vilivyotokea usiku wa kuamkia jana Mikumi mkoani Morogoro.

Wasanii hao walikumbwa na mkasa huo wakiwa safarini kutoka ziara ndefu maalum ya mikoa ya Nyanda za Juu Kusini. Katika ziara hizo, wasanii hao walitumbuiza katika mikoa ya Iringa, Mbeya na na Ruvuma mjini Songea.

Akizungumza mwenyekiti wa kamati maalum ya mazishi ambaye pia ni mlezi wa kundi la Jahazi Modern Taarab aliyetambulishwa kwa jina la Ferouz Juma alisema fani ya muziki huo imepata pigo kubwa.

Vilio hivyo jana vilitanda kwenye ukumbi wa baa maarufu ya Ikweta Grill, Mtoni jijini Dar es Salaam, mahali ambako miili ya marehemu hao ililetwa kutoka Morogoro tayari kwa mazishi huku ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu hao wakiwa wamekusanyika kwa wingi wakisubiri kupokea miili ya wapendwa wao na kwenda kuisitiri.

Kamati maalum ikiongozwa na Ferouz na Mbunge wa Kinondoni, Idd Azan ilitangaza harambee ya kuchangia fedha kwa ajili ya kusaidia familia za marehemu hao.

Mkurugenzi wa Five Stars, Hamis Slim alishindwa kuzungumza na kusema: "Sina la kusema, sijui niseme nini, ni msiba usioelezeka, nimepoteza wasanii
wangu karibu wote, siamini mpaka sasa hiki kilichotokea, Mungu pekee ndiye anaywejua, ni msiba usioelezeka sijui kama nitaweza kusahau katika maisha yangu yote."

Waziri wa Habari, Vijana , Utamaduni na Michezo, Dk Emmanuel Nchimbi alisema: Kwa niaba ya serikali nasema familia ya taarabu nchini imepata msiba mzito sana, ni msiba wa taifa kwa kweli, serikali tumeupokea kwa mshtuko mkubwa, tunaungana na familia zote katika kipindi hiki kigumu."

Naye Abood Aziz ambaye ni Mbunge wa Morogoro alitoa magari maalum kwa ajili ya kusafirishia maiti za marehemu wasanii hao tayari kwa mazishi.

Mama mzazi wa msanii Issa Kijoti, Amina Said akilia alisema: "Mwanangu aliniaga Jumatano iliyopita akaniambia mama mi nasafiri Nasra huyo
mama niangalizie mlee vizuri mama, mi narudi Jumatatu, akaniachia na fedha, kumbe mwanangu ndo alikuwa ananiaga, siamini kama Issa amekufa, jamani mimi nimeumbuka, nani atanisaidia jamani mimi....

"Nilikuwa namtegemea mwanangu kwa kila kitu yeye ndio msaada wangu pekee, kaondoka na miguu yake akiwa na furaha tele, leo anarudi kwenye jeneza na kuniacha mkiwa mimi jamani,"alilia kwa kwikwi.

Kijoti alitarajiwa kuzikwa jana kwenye makaburi ya Mtoni Relini, na ameacha mtoto wa kike wa miaka mitatu aitwae Nasra.

Mjomba wa marehemu OmaryAbdallah aliyejitambulisha kwa jina la Hatha Bui alisema, "Omary amekufa akiwa mdogo sana miaka 25, alikuwa mtoto wa pekee wa kiume kwa dada yangu kati ya watoto wake tisa, mazishi tumepanga yatafanyika kijiji cha Magawa Kisiju,"

Msanii wa kundi hilo aliyenusurika Joha Kassim alisema: "Ni msiba mzito sitaweza kuusahau katika maisha yangu, ni Mungu pekee ndio anayejua kwani kama si kuumwa ungekuta na mimi nipo kwenye msafara huo.

Naye Hadija Kopa alisema: "Msiba hausemeki, nimeanza nao Zanzibar Stars ingawa nilikuwa na kundi langu la TOT, ikawa Five Stars safari nilitakiwa niwepo bahati mbaya kikundi changu kilianza shoo, huwezi kuamini mtu aliyewapeleka Songea alinipigia
simu ili Jumapili niwepo kule (Songea), lakini nilikataa kutokana na majukumu ya kazi kwenye kikundi changu, jamani Mungu,"alishindwa Kopa na kisha kuangua kilio.

Omary Tego: Nimepokea kwa masikitiko makubwa nakumbuka Five Stars wapo waliotoka kundi langu la Coast Modern Taarab, wasanii watano waliotoka kwangu mmoja ,Ally Jay ndiye amenusurika wengine wote wamefariki, ni msiba mzito sijui nisemeje."

Asha Baraka, ambaye ni Mkurugenzi wa African Stars, Twanga Pepeta: :"Huu msiba sio wa Slim na ndugu wa marehemu peke yao ni msiba wetu
sote jamii ya muziki na wapenda burudani, kupitia kamati yetu maalum ya mazishi inayoongozwa na Ferouz na mbunge Idd Azan, tunaomba wadau mbalimbali watuchangie ili tuweze kuwafariji wafiwa, ajali hii ni ya kitaifa.

Tunaomba michango kama ile ya Gongo la Mboto msituachie wasanii wenyewe, haijapata kutokea msiba kama huu,"alisema Asha Baraka na tayari wadau mbali mbali wameshaanza kutoa rambi rambi zao mpaka jana mchana tayari Shilingi 1.7milioni zilikuwa zimeshapatikana, kati ya hizo Shilingi 1.5 m zikitolewa ahadi.

Kundi hilo la Five Stars likiongozwa na Issa Kijoti litakumbukwa na nyimbo zao kama Wapambe Msitujadili, Riziki Mwanzo wa Chuki, Uzushi Haunitii doa na Alonacho Kajaliwa. Wimbo ulikuwa unatamba ni Msitujadili 'Mchumu....Mchumu tena mwaa."

Picha na habari zaidi tembelea http://www.didamitikisiko.blogspot.com/

No comments:

Post a Comment