.

.

.

.

Tuesday, March 29, 2011

WAKALA AJIPATIA MABILIONI KUPITIA NHC

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Maliasili, Ardhi na Mazingira imebaini kuwapo kwa mtu aliyekuwa akihodhi nyumba 30 za Shirika la Taifa la Nyumba (NHC) huku akizitumia kujipatia takribani Sh milioni 525 kwa mwezi kutoka kwa watu aliopangisha.

Taarifa juu ya wakala huyo ambaye hata hivyo Mwenyekiti wa Kamati, James Lembeli, na
uongozi wa NHC hawakuweka jina lake hadharani mbele ya waandishi wa habari, ilitolewa wakati wa kuelezea changamoto zinazolikabili shirika hilo.

Akikariri taarifa kutoka kwa uongozi wa shirika, Lembeli alisema mtu huyo alikuwa akihodhi nyumba hizo eneo la Masaki, Dar es Salaam na mkataba wake ulisitishwa Januari.

Kamati na uongozi wa shirika, pia hawakuweka bayana undani wa mkataba huo; muda na maudhui yake.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari baada ya kufanya mazungumzo na uongozi wa NHC, Lembeli alisema wakati mtu huyo alikuwa akiwasilisha dola 15,000 (Sh milioni 225) za Marekani kwa NHC kila mwezi, binafsi alikuwa akibakiwa na dola 50,000 (Sh milioni 750) kila mwezi.

Katika kile ambacho Mwenyekiti huyo wa Kamati alisema ni matokeo ya mikataba mibovu kati ya NHC na wapangaji wake, alisema kwa mwaka, wakala huyo alijipatia dola 600,000 (Sh milioni 900) dhidi ya dola 180,000 (Sh milioni 270) alizowasilisha NHC.

“Naomba muwe wakali. Serikali isiwatetee. Tatizo wengi wa wapangaji wa Shirika la Nyumba ni wastaafu, wafanyabiashara wakubwa na watumishi wenye nyadhifa,” alisisitiza Lembeli.

Mwenyekiti huyo alisisitiza, “kama kuna wengine wa aina hii, zichukuliwe hatua. Naamini wapo wengine wanaohodhi nyumba na kukodisha kwa wengine.

Kwa nini haya yatokee kwenye taasisi za Serikali?” Alihoji. Kamati hiyo ililitaka Shirika kuhakikisha linaingia mikataba yenye tija na uwezo wa kuwabana wapangaji, kuhakikisha haitoi mianya ya kulifikisha mahakamani.

Kwa mujibu wa Lembeli, zipo kesi zaidi ya 200 kati ya NHC na wapangaji ambazo ni matokeo ya mikataba mibovu.

Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemiah Mchechu, alisema mkataba wa wakala huyo ulisitishwa na nyumba kurudishwa kwa Shirika tangu Januari.

Mchechu ambaye alishika wadhifa huo Aprili mwaka jana, hata hivyo alipongezwa na kamati hiyo kwa kilichoelezwa kwamba tangu aongoze shirika, baada ya miezi minne, yapo mabadiliko makubwa chanya yaliyojitokeza.

Miongoni mwa mambo yaliyopongezwa kufanywa na uongozi huo mpya, ni pamoja na ongezeko la makusanyo ya madeni ambayo kulingana na taarifa iliyotolewa, hadi Novemba mwaka jana, Shirika lilikuwa na Sh bilioni 1.5 benki lakini sasa zipo Sh bilioni nane.

“Wabunge wamekubali, watendaji ni wazuri, wana uwezo na nia ya kufanya kazi… sana sana ni
vijana,” alisema Lembeli na kuitaka Serikali isiliingilie Shirika kwa kutumia wanasiasa ambao kwa mujibu wake, wamesababisha mashirika mengi kufa.

Wakati huo huo, Mchechu alisema leo wanaanza operesheni ya kuwaondoa wadaiwa sugu walioshindwa kulipa malimbikizo ya kodi.

Deni linalodaiwa kutoka kwa wapangaji ni Sh bilioni 4.8. Kamati ya Bunge ilishauri majina ya wadaiwa wakubwa na kiasi cha fedha wanazodaiwa viwekwe hadharani.

Katika hatua nyingine, Kamati iliishauri Serikali kufanya mabadiliko ya Sheria iliyounda NHC ili kuiwezesha kukopa benki bila kulazimika kupata kibali cha Hazina, ili iongeze kasi ya ujenzi wa nyumba za kuuza.

Kwa mujibu wa Kamati, ombi hilo linazingatia kwamba mkakati wa ujenzi wa nyumba 15,000 ndani ya miaka mitano, unahitaji kasi, jambo ambalo upo wasiwasi kwamba hatua ya kusubiri kibali cha Wizara, inaweza kulikwamisha.

Ilitaka mabadiliko hayo ya Sheria namba 2 ya mwaka 1990 iliyounda NHC pia yaiondolee Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) wakati wa kuuza nyumba hizo, ili kukidhi malengo ya kuziuza kwa bei nafuu.

No comments:

Post a Comment