.

.

.

.

Saturday, April 09, 2011

MAKAMBA AFIKA NJIA PANDA

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),Yusuf Makamba


HATMA ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuf Makamba inatarajiwa kujulikana kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho kinachoanza leo.

Kikao hicho kinaanza asubuhi hii mjini hapa, huku kukiwa na taarifa kuwa sekretarieti yake huenda ikavunjwa.
Taarifa kutoka vyanzo mbalimbali vya ndani ya CCM, zinadai kuwa uamuzi huo unachukuliwa ikiwa ni hatua ya chama hicho kujivua gamba linaloonekana kuchuja mbele ya umma.

Chanzo chetu cha habari kilidai kuwa, baada ya kuvunjwa sekretarieti, Makamba ambaye ndiye mwenyekiti wa sekretarieti hiyo, atawasilisha taarifa ya kuomba kustaafu.Hatua hiyo inamwezesha Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete kuteua sekretarieti nyingine ambayo itakiongoza hadi mkutano mkuu unatarajiwa kufanyika mwakani.

Makamba amekuwa akituhumiwa kusababisha chama hicho kufanya vibaya kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita.
Anatuhumiwa kutoa kadi kwa baadhi ya wagombea wa chama hicho ambazo zilitumika kuingiza wanachama mamluki na kuruhusu kila mwanachama wa CCM kupiga kura ya maoni.

Halmashauri kuu ilikuwa imeagiza kura za maoni ndani ya chama hicho zihuhusishe wanachama hai, lakini aliagiza kila mwanachama kushiriki bila kujali kama ni hai au hajalipia kadi yake.

Kulingana na kanuni za chama hicho, iwapo sekretarieti hiyo itavunjwa, licha ya Makamba watakaopoteza nafasi zao ni Naibu Makatibu wakuu CCM bara na Zanzibar, George Mkuchika na Saleh Ramadhan Ferouz, Katibu wa Itikadi na Uenezi, John Chiligati; Katibu wa Mipango, Kidawa Saleh na Katibu wa Kitengo cha Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.

Wanaotajwa kuchukua nafasi ya Makamba ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi na Waziri wa Habari, Ajira, Utamaduni na Michezo, Dk Emmanuel Nchimbi huku ikidaiwa kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Abdulrahman Kinana amekataa nafasi hiyo. Mwingine anayetajwa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira lakini inadaiwa kuwa kasoro inayomkumba ni pale alipokihama chama hicho na kwenda NCCR-Mageuzi.

Akipokea wanachama wapya kutoka Chadema jana, Rais Kikwete alisema kikao hicho ni muhimu kwa chama chao huku akiwaomba radhi wanachama kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu na kuwataka wasahau yaliyopita, wagange yajayo.

“Tunaanza vikao muhimu vya kujenga chama chetu,” alisema Rais Kikwete.Wanachama wapya waliojiunga na CCM ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mbeya, Shambwele Shitambala na Katibu Mwenezi wa Chadema Wilaya Ileje, Henry Sayuni.Rais Kikwete alisema Tanzania ina vyama vingi, lakini ukweli utabaki kuwa CCM ndicho makini huku akisema vingine siyo vyama, bali mkusanyiko wa wanaharakati.

No comments:

Post a Comment