.

.

.

.

Thursday, April 21, 2011

MRISHO NGASSA KURUDI YANGA !!!


MSHAMBULIAJI wa zamani wa Yanga anayekipiga Azam FC, Mrisho Ngassa amesema yuko tayari kurejea Yanga lakini endapo tu viongozi wa pande zote mbili watakaa pamoja na kukubaliana maslahi.

Hatua ya Ngassa imekuja baada ya kuwepo na habari kuwa Yanga wanataka kumrudisha mshambuliaji wao huyo aliyenunuliwa na Azam FC kwa mkataba wa sh58mil msimu uliopita.

Yanga iliyotwaa ubingwa wa Tanzania Bara, iko katika mchakato wa kukifumua kikosi chake kujipanga upya kwa ajili ya michuano ya Ligi Kuu msimu ujao na Ligi ya Mabingwa Afrika, ambayo Yanga ina tiketi yake.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili Yanga, Seif Ahmed amepewa jukumu la kuhakikisha inasukwa Yanga imara yenye ushindani kwa kuondoa baadhi ya wachezaji, kuongeza na kuwabakisha wengine.

Kwa kuanzia, Yanga imewasajili wachezaji kadhaa akiwemo Godfrey Taita wa Kagera Sugar, mshambuliaji wa zamani wa Simba, Pius Kisambale na kipa wa Majimaji ya Songea, Said Mohamed.

Lakini, wakati Yanga ikifanikisha upande huo, Ngassa alisema kuwa kwa upande wake hawezi kuliongelea sana suala hilo la kurudi Yanga kwa kuwa bado ana mkataba na Azam.

''Siwezi kuongelea sana suala hilo ila kwa kuwa mimi nina mkataba na Azam, sasa kama Yanga wananitaka nirudi basi wanatakiwa waongee na viongozi wangu wakikubaliana mimi niko tayari kwani ninachoangalia ni maslahi,'' alisema Ngassa.

Lakini Ngassa aliongeza kuwa kwa upande wake mpaka sasa hakuna kiongozi yoyote aliyemfuata kufanya naye mazungumzo hivyo hawezi kuliongelea sana kwani hajui chochote kinachoendelea.

Habari zilizopatikana hivi karibuni zilieleza kuwa klabu hiyo ya Yanga imetenga mamilioni ya fedha za kusajili wachezaji wapya na wenye uwezo mkubwa akiwemo Ngassa ili kuongeza nguvu katika kikosi chao cha msimu ujao.

Mbali na Ngassa, mwalimu wa timu hiyo, Sam Timbe aliwasilisha ripoti yake kiutaka uongozi wa Yanga kuhakikisha unasajili wachezaji wengi wa nje kwa ajili ya kupata Yanga imara, ya ushindani kwa michuano ya kimataifa.

Timbe aliyerithi mikoba ya Kosta Papic, raia wa Serbia, aliichukua Yanga katika kipindi kifuupi na kuipa mafanikio kwa kutwaa ubingwa kabla ya kuondoka kurudi Uganda atakakokuwa huko kwa miezi miwili.

No comments:

Post a Comment