MBUNGE wa Bunge la Tanzania kupitia Baraza la Wawakilishi, Mussa Khamis Silima (60), amefariki dunia leo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam.
Mbunge huyo wa jimbo la Msufini na familia yake walipata ajali ya gari juzi usiku Nzuguni mkoani Dodoma, mkewe, Mwanaheri Twalib (48) alikufa papo hapo, amezikwa jana Zanzibar.
Spika wa Bunge, Anne Makinda amewatangazia wabunge kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii , Blandina Nyoni amemuarifu kuwa Silima ameaga dunia.
Makinda ameahirisha shughuli za Bunge hadi kesho saa tatu asubuhi ili kutoa fursa kwa wabunge kuomboleza kifo cha mwenzao.
Leo asubuhi baada ya dua ya kuliombea Bunge na kuiombea nchi yetu, Makinda aliwaeleza wabunge kuwa, alizungumza na Silima, na kwamba alikuwa anaendelea vizuri.
Baada ya taarifa hiyo ya Spika kuhusu kifo cha Mbunge huyo, wabunge walisimama kwa dakika moja kumbuka marehemu Silima.
“Mwenyezi Mungu aipumzishe roho yake mahali pema peponi, amina” amesema Spika wa Bunge na kuitaka Kamati ya Uongozi ya Bunge na Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii wakutane kuzungumzia ushiriki wa Bunge katika msiba huo.
Makinda, jana aliwatangazia wabunge kuwa, Mbunge huyo na wenzake walipata ajali saa mbili kasorobo usiku, Silima aliumia, akalazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma. Kwa mujibu wa Makinda, Silima alipata majeraha makubwa.
Kwa mujibu wa Makinda, Mbunge na familia yake walikuwa wanarudi Dodoma wakitoka Zanzibar kumzika kaka wa mke wa Mbunge huyo.
Gari lililopata ajali aina ya Toyota Corolla liliharibika vibaya, lilivutwa juzi usiku likiwa halina baadhi ya matairi, lipo kwenye kituo kikuu cha Polisi Usalama Barabarani Mkoa wa Dodoma.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Zelothe Stephen, gari alilokuwa akisafiria Silima liligongana na magari mengine mawili saa 2.15 usiku katika barabara kuu ya Dodoma- Morogoro nje kidogo ya manispaa ya Dodoma.
Kamanda huyo amesema, gari hilo lenye namba za usajili T.509 AJC lilikuwa likitoka upande wa Morogoro kuelekea mjini Dodoma, kulikuwa na watu wanne ndani ya gari hilo akiwemo aliyekuwa akiliendesha, Chezard Sebunga (31), mkazi wa Chinangali Manispaa ya Dodoma, Silima, Mwanaheri mkazi wa Zanzibar, na Salama Juma (50) mkazi wa Area ‘D’ Manispaa ya Dodoma.
Gari hilo liligonga lori lenye namba T. 330 AYF aina ya Isuzu likiwa na tela lenye namba za usajli T. 673 ATS upande wa kulia kwenye gurudumu la nyuma kabisa kulia na kuyumba kisha kugonga lori linguine aina ya Scania lenye namba za usajili T. 497 ASW lililokuwa likitoka mjini Dodoma kuelekea Morogoro.
Kwa mujibu wa Polisi, chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari alilokuwa akisafiria Mbunge huyo kwa kuwa hakuwa mwangalifu wakati akitaka kulipita gari lililokuwa mbele yake akiwa katika mwendo kasi
No comments:
Post a Comment