.

.

.

.

Friday, August 19, 2011

MULTICHOICE YATOA MSAADA KWA YATIMA

Na Ismail Ngayonga

MAELEZO

Dar-Es-Salaam

KAMPUNI ya ving’amuzi nchini Tanzania ya Multichoice imewafuturisha watoto yatima wanaolelewa katika kituo cha Al-Madina kilichopo Tandale kwa tumbo na kuitaka jamii kuwatunza na kuwalea watoto hao.

Akitoa salamu za shukrani kwa niaba ya kampuni hiyo jana jioni, Meneja uendeshaji wa Multichoice Tanzania Bw. Ronald Shelukindo alisema ofisi yake imefurahishwa na jitihada zinazofanywa na kituo hicho katika kuwalea watoto yatima.

Shelukindo alisema Multichoice Tanzania imeguswa na changamoto mbalimbali ilizojionea katika kituo hicho, hivyo kwa kutambua jukumu la kusaidia watoto yatima yatima ofisi hiyo imekusudia kuwasaidia kwa kadri inavyowezekana.

“Binafsi nimeguswa na hali ya watoto hawa hususani tulipojumuika nao katika futari hii, hivyo nitazungumza na marafiki zangu katika kuangalia namna ya kusaidia malipo ya pango la nyumba katika kituo hiki” alisema Shelukindo

Aidha aliwataka watoto kuwa na maadili mema katika jamii kwa kutambua kuwa malezi wanayopatiwa katika kituo hicho yapo katika usimamizi wa misingi ya dini ambayo yanakataza kutenda matendo mabaya.

Naye Meneja Mawasiliano wa Multichoice Tanzania, Bi. Barbara Kambogi alisema katika kuonyesha mapenzi waliyonayo kwa watoto hao, kampuni hiyo pia imetoa msaada wa nguo, jiko la gesi pamoja king’amuzi chenye chaneli za dstv ili kuwaburudisha watoto hao katika siku za mapumziko.

‘’Kwa kuwa watoto hawa wapo katika umri na lika tofauti kwa mfano wavulana walio wengi wao ni wapenzi wakubwa wa mchezo wa mpira wa miguu, hivyo king’amuzi hiki kitakuwa ni kiburudisho kwao’’ alisema Kambogi.

Kwa upande wake Mlezi wa Kituo hicho, Bi. Kuruthum Yusuph alisema kituo hicho kilianzishwa rasmi mwaka 2004 kikiwa na watoto wakiwemo wavulana 4 na wasichana wenye umri kati ya miaka 6-10.

Bi. Kuruthum aliitaka jamii kuwa haina budi kusaidia makundi ya watu wasioweza ikiwemo watoto yatima, ambapo katika miaka ya hivi karibuni idadi yao inazidi kuongeza siku hadi siku.

“Kutoa ni moyo na si utajiri, wapo watu wenye uwezo mkubwa wa kuwasaidia watoto yatima lakini kwa sababu ama nyingine wameshindwa kufanya hivyo, kwa niaba ya watoto hawa natoa shukrani za dhati kwa multichoice Tanzania” alisema Bi. Kuruthum

Aidha aliiomba Serikali kukisaidia kituo hicho, hususani katika suala la malipo ya ada kwa wanafunzi wanaosoma katika shule za msingi na Sekondari kwani idadi yao imekuwa ikiongezeka kila mwaka.

Alisema kituo hicho kinawalelea watoto yatima wenye umri katika ya miaka 2 hadi 17, hivyo suala la huduma za kijamii ikiwemo elimu ni suala lisiloweza kuepukika.

No comments:

Post a Comment