.

.

.

.

Tuesday, November 22, 2011

AUZIA WATU NYAMA YA MBWA

POLISI mkoani Singida wamemkamata mtu kwa madai ya kukutwa na nyama ya mbwa ambayo anasadikiwa kuwauzia watu mbalimbali mjini Singida.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Mrakibu Mwandamizi Ayoub Tenge alimtaja mtuhumiwa kuwa ni Eliud Abdallah (32) mkazi wa eneo la Misuna, Halmashauri ya Singida na alikamatwa Novemba 17, mwaka huu ya saa 10 jioni.

Akielezea mkasa huo, Tenge alisema siku ya tukio, baadhi ya watu wa eneo anakoishi walitilia shaka uhalali wa kitoweo ambacho mtuhumiwa alikuwa anakiuza mara kwa mara mitaani na hivyo kutoa taarifa Polisi.

Alisema, baada ya mtuhumiwa kuhojiwa, alikiri kuwa huiuza nyama hiyo kwa wateja wake mbalimbali wa kudumu, hususan watengeneza supu katika vilabu vya pombe za kienyeji.

Kilo moja huiuza kwa Sh 2,000 tu. Aidha, mtuhumiwa huyo alibainisha kuwa mbwa hao huwapata mitaani ambapo huwadanganyishia chakula hadi kufanikiwa kuwakamata.

Katika tukio lingine, mkunga wa jadi, Hawa Athuman (53) mkazi wa Kijiji cha Masweya, Singida Vijijini, anadaiwa kuua kichanga cha siku mbili kwa kukiziba kwa nguo usoni hadi kuishiwa pumzi.

Kaimu Kamanda alisema mauaji hayo yalifanyika katika Hospitali ya Mkoa wa Singida, Novemba 19, mwaka huu saa sita mchana.

Alieleza kuwa siku ya tukio, Hawa alienda hospitalini hapo kwa madhumuni ya kwenda kumuona jirani yake, Amina Iddi (36), ambaye alikuwa amejifungua kitoto hicho.

Tenge alidai mtuhumiwa huyo baada ya kufika wodini, alimuomba mama wa kichanga hicho akifanyie dua, kitendo ambacho kilisababisha kifo cha kichanga hicho kutokana na kukifunika gubigubi hadi kukosa hewa.

No comments:

Post a Comment