.

.

.

.

Friday, November 11, 2011

MH.FREEMAN MBOWE AACHIWA KWA DHAMANA


MWENYEKITI wa Taifa Chadema, Freeman Mbowe, amepandishwa kizimbani katika Mahakamani ya Hakimu Mkazi Arusha na kusomewa mashtaka mawili ya kufanya mkusanyiko kinyume cha sheria na kukataa kutii amri halali ya polisi iliyowataka kutawanyika.

Kutokana na mashitaka hayo, Mbowe ameunganishwa na washtakiwa wengine 27 wanachama wa chama hicho, waliofikishwa mahakamani hapo Jumanne iliyopita wakikabiliwa na mashtaka kama hayo, akiwemo Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu .

Mbowe ambaye pia Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzania Bungeni, ameunganishwa kwenye kesi hiyo ya jinai namba 454/2011 ambapo watuhumiwa wote kwa kwa pamoja, wanadaiwa kufanya kusanyiko isivyo halali katika viwanja vya NMC, eneo la Unga Ltd, Manispaa ya Arusha Novemba 7 mwaka huu.

Hata hivyo Mbowe ambaye anakuwa mshitakiwa wa 28 kwenye kesi hiyo, alikana mashitaka yote mawili yaliyosomwa mahakamani hapo na Wakili wa Serikali Haruna Matagane akisaidiwa na mwenzake, Agustino Kombe.

Upande wa utetezi ukiongozwa na mawakili Method Kimomogoro na Issa Rajabu, uliiomba mahakama hiyo kumpa dhamana mteja wao kwa masharti sawa na wenzake.


Hakimu Devotha Kamuzora anayesikiliza kesi hiyo, alikubaliana na maombi hayo na kumpa dhamana Mbowe, kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili wenye vitambulisho na barua ya utambulisho kutoka kwa Ofisa Mtendaji wa Kata ambao walitia saini hati ya dhamana ya Sh milioni tano kila mmoja.

Mwenyekiti huyo aliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti . Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 22, mwaka huu itakapotajwa.

No comments:

Post a Comment