.

.

.

.

Friday, November 18, 2011

MIKOPO YA NYUMBA KUTOKA BENKI YA AFRIKA

BANK of Africa (BOA) Tanzania imezindua huduma ya mikopo ya nyumba ambayo Watanzania watakopa na kujipatia nyumba za kisasa kwa ajili ya familia zao na pia kujipatia kipato kuondokana na hali duni ya maisha.

Akizindua mkopo huo Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mwendeshaji wa benki hiyo, Ammish Owusu-Amoah alisema uzinduzi huo unalenga kuwasaidia Watanzania kupata makazi bora, vipato na kuunga mkono sera ya Serikali wananchi kuwa na makazi bora.

“Leo hii, sisi Bank of Africa tumefarijika sana kuzindua mkopo wa nyumba kwa ajili ya wateja wetu na Watanzania wengine kama njia ya kuunga mkono Serikali sera ya maisha bora kwa Watanzania,” alisema.

Alisema wiki mbili zilizopita, benki hiyo ilisaini makubaliano pamoja na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na wadau wengine wa kampuni za Victoria Plaza na Real Estate, ambapo walikubaliana kuhusu mkopo huo.

Alisema benki inatoa mikopo ya aina tatu ambapo mkopo wa kununua nyumba unatolewa kwa asilimia 80 ya thamani ya nyumba husika popote ilipo.

Alisema pia mkopo mwingine unatolewa kwa ukarabati wa nyumba iliyojengwa lakini haikukamilika kutokana na kukosa fedha, hivyo benki inatoa mkopo ili kuikamilisha.

Alisema mkopo wa tatu unaotolewa ni wa asilimia 50 ya thamani ya nyumba husika ambayo tayari imekamilika kwa ajili ya kumwezesha mwenye nyumba kupata mkopo kuanzisha biashara au shughuli yoyote ya maendeleo ili kujiongezea kipato.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa BOA Tanzania, Balozi Fulgence Kazaura alisema taasisi hiyo imeonesha umuhimu wa kuwa na nyumba na hivyo kuongeza uwezo wa kujiendeleza miongoni mwa Watanzania.

Balozi Kazaura alisema mikopo hiyo inalenga kumsaidia Mtanzania wa ngazi yoyote kimaisha na kwamba masharti ya kupata mkopo huo ni rahisi.

Mkurugenzi wa Biashara wa NHC, David Shambwe alisema amefurahi kuona benki hiyo ikiamua kujiunga kwenye soko la watoaji bidhaa kwa Watanzania kununua nyumba na kwamba shirika lake linazalisha nyumba na linaendelea kuzalisha nyumba kwa watu wa vipato mbalimbali nchini.

Alisema mikopo hiyo imekuja katika muda mwafaka maana Watanzania wakikopa fedha hizo itawezesha kununua nyumba ambazo zinajengwa na NHC.

Alitoa mwito kwa Watanzania kuanza kutembelea matawi ya benki hiyo nchini ili wapate mikopo ya kununua nyumba zinazojengwa na shirika hilo.

No comments:

Post a Comment