.

.

.

.

Wednesday, December 28, 2011

KESHO HADI JUMAMOSI DSM KUKUMBWA NA MAFURIKO MAKUBWA ZAIDI (UTABIRI)


MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imetoa tahadhari ya kuendelea kunyesha mvua kubwa zaidi katika siku 10 zijazo, huku ikizitaja Alhamisi hadi Jumamosi kuwa ni siku za mafuriko mengine makubwa zaidi katika jiji la Dar es Salaam.
Wakati TMA ikitoa tahadhari hiyo, Shirika la Reli Tanzania (TRL), limesitisha safari za treni ya abiria kwa muda usiojulikana kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma, kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali ya nchi.
Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Agnes Kijazi alisema jana katika taarifa yake kuwa kutokana na mvua hizo, ni vyema tahadhari zote zikachukuliwa mapema ili kuepuka maafa zaidi.
“Wale wananchi ambao wanaishi mabondeni na waliokumbwa na mafuriko, wahame kutokana na mvua zinazoanza kunyesha Desemba 27 (jana), hadi Desemba 31 mwaka huu, kwani zitaleta madhara makubwa kwa wanaoishi mabondeni na sehemu nyingine mbalimbali,” alisema Dk Kijazi.
Alisema kwamba ukanda wa mvua unatarajia kuimarika maeneo mengi nchini na mvua zinatarajiwa kuanza kwenye ukanda wa pwani, ikiwemo Mkoa wa Dar es Salaam na kuongezeka kuelekea mwaka mpya wa 2012.
Dk Kijazi alisema mifumo ya hali ya hewa inaonyesha kuimarika kwa hali ya joto katika Bahari ya Hindi na kuongezeka kwa msukumo wa hewa yenye unyevunyevu kutoka misitu ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC).
Alisema hali hiyo imesababisha makutano ya upepo katika eneo la Mashariki na Kusini Magharibi mwa nchi, kuanzia leo kuelekea mwaka mpya... “Hali hii inatarajia kusababisha kuanza kwa vipindi vya mvua kubwa katika maeneo mengi hapa nchini.”
Alisema maeneo ya mikoa ya ukanda wa Pwani (Dar es Salaam, Pwani, Mtwara, Lindi na Unguja), yanatarajiwa kuwa na vipindi vya mvua kubwa.
Dk Kijazi aliyataja maeneo mengine kuwa ni ya Nyanda za Juu Kusini Magharibi ambayo ni Mikoa ya Mbeya, Iringa na Rukwa na Kanda ya Kati katika Mikoa ya Dodoma na Singida.
“Kwa upande wa Magharibi mwa nchi, Mikoa ya Kigoma na Tabora na maeneo machache ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki katika Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara, yanatarajiwa kuwa na vipindi vya mvua kubwa,” alisema.
Alisema kutokana na viwango vikubwa vya mvua vilivyonyesha, ongezeko kidogo la mvua linatarajia kusababisha mafuriko na uharibifu wa miundombinu, hivyo ni muhimu tahadhari stahili ziendelee kuzingatiwa.
Msimbazi wagoma
Licha ya tahadhari hiyo ya TMA, baadhi ya wakazi waishio katika Bonde la Mto Msimbazi wamedai kuwa hawataondoka katika nyumba zao zilizokumbwa na mafuriko hadi watakapoona maji yamejaa katika mto huo.
Wakizungumza jana kwa nyakati tofauti wakazi hao walisema hawana pa kwenda licha ya kuisikia tahadhari hiyo ya TMA.
“Ningekuwa mpangaji sawa, sasa mimi nimejenga nitakwenda wapi na kwetu ni mikoani huko,” alisema Ramadhani Kimbuyu wakati akifanya ukarabati wa nyumba yake huku akisisitiza kuwa kipimo chao kitakuwa Mto Msimbazi.
Alisema kosa walilofanya awali ni kupuuza licha ya kuona mto huo umejaa jambo ambalo alidai hawatalirudia... “Tukiona yamejaa tu tunahamia juu relini, yakipungua tunarudi.”
Kauli ya RC
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki amesema Serikali itawachukulia hatua kali watakaokaidi amri ilivyotangazwa na Rais Jakaya Kikwete ya kutorejea katika maeneo hatarishi ya mabondeni.
“Tangu mwaka 1979 Serikali ilitoa amri ya watu kuondoka mabondeni lakini wamekuwa wakikaidi na kuendelea kuishi,  kitendo hicho kimechangiwa na uzembe kwa baadhi ya viongozi katika kutekeleza agizo hilo,” alisema.
Sadiki alisema baadhi ya watu wameanza kurejea kwenye mabonde yaliyoathirika na kuwaonya wasirudi na badala yake watafute maeneo mengine kuendesha makazi yao.
Alisema Serikali itawapatia waliojenga mabondeni viwanja na siyo wapangaji. Wakazi hao wametengewa viwanja katika eneo la Mabwe Pande lililoko mpakani na Bagamoyo, Pwani na kwamba mpaka sasa viwanja 700 vimeshapimwa.
“Baada ya kugawa viwanja hivi tutaanza zoezi la kuzibomoa nyumba walizokuwa wanaishi maeneo ya mabondeni ili kutoruhusu watu kurudi tena huko kwani bila kufanya hivyo, hatutafanikisha lengo hilo,” alisema Sadiki.

No comments:

Post a Comment