.

.

.

.

Tuesday, June 26, 2012

.MABILIONI YA VIGOGO WA TANZANIA ZIKO KATIKA MABENKI YA USWISI


.

KITENGO cha Polisi wa Kimataifa (Interpol) nchini kinachunguza Sh303.7 bilioni ambazo zinadaiwa kukutwa kwenye akaunti sita za Watanzania, wakiwamo wanasiasa, katika benki mbalimbali nchini Uswisi.

Chanzo cha habari cha kuaminika  kutoka ndani ya Interpol kilichonukuliwa na gazeti dada la Mwananchi, The Citizen, kimesema baadhi ya wanasiasa nchini na watu wengine ndiyo wanahusika na ufisadi huo kwa kuwa na akaunti zenye fedha nyingi nchini Uswisi.
Fedha hizo zimeelezwa ziliingizwa katika akaunti hizo na kampuni za uchimbaji mafuta na kampuni za uchimbaji madini, ambazo zinafanya kazi Tanzania.

Chanzo hicho kiliongeza kwamba fedha hizo zipo katika akaunti sita tofauti, zinazomilikiwa na Watanzania wakiwamo wanasiasa.

Kiasi hicho cha fedha kilichofichwa Uswisi, kinatosha kuendesha Bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa miaka mitano, au kusaidia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, kuendesha shughuli zake kwa miaka miwili.

Hata hivyo, chanzo hicho kilieleza kuwa tangu akaunti hizo zifunguliwe wamiliki wake halali hawajawahi kuingiza hata shilingi moja.

"Wenzetu wa Uswisi wameeleza fedha hizo zimeingizwa na kampuni kadhaa ambazo zinahusika na mafuta pamoja na madini hapa nchini," kilidokeza chanzo hicho.

Mabilioni hayo yamebainika kufichwa wakati takwimu zilizotolewa na Umoja wa Taasisi za Kupambana na Rushwa barani Afrika ikiwamo Tanzania, zikionyesha kwamba Sh22 trilioni, zimekuwa zikitoroshwa nchini humo na kufichwa katika nchi za kigeni, ikiwamo Uswisi.

 Fedha hizo zimebainishwa na ripoti ya Benki ya Taifa ya Uswisi (SNB), iliyotolewa hivi karibuni, ikibainisha nchi mbalimbali ikiwamo Tanzania, na kiwango cha fedha zake zilizohifadhiwa huko.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) hivi sasa inafuatilia suala hilo kwa mamlaka za Uswisi, ili kujua fedha hizo ziliko na nani anazimiliki.

CHANZO: MWANANCHI


.

No comments:

Post a Comment