.

.

.

.

Saturday, August 11, 2012

AJALI MBAYA YAUA 12 HAPO HAPO



Baadhi ya abiria walionusurika wakiwa katika eneo la tukio kabla ya kupata msaada



WANAKWAYA 12 raia wa Kenya wamekufa papo hapo jana baada ya magari waliyokuwa wakisafiria kupata ajali katika Kijiji cha Makole jirani na Mto Wami na kuhusisha magari manne.

Katika tukio la ajali, wanakwaya hao 12 walikufa na wengine 25 walijeruhiwa vibaya baada ya magari manne yakiwemo mawili ya abiria yaliyowabeba wanakwaya hao kupinduka na lingine kugongwa na lori ambalo nalo liligonga lori lingine baada ya kusababisha ajali hiyo.

Aidha habari kutoka nchini Kenya zinapasha kuwa Rais wa Kenya, Mwai Kibaki ametuma ndege ya kuwabeba majeruhi wa ajali hiyo na kuwakimbiza Kenya kwa matibabu zaidi.

Akizungumzia chanzo cha ajali, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Ernest Mangu alisema  ajali hiyo ilitokea saa 11 alfajiri jana  ambapo lori la mizigo lililokuwa likitokea Tanga kuelekea Dar es Salaam liligonga basi dogo la abiria lililowabeba wanakwaya hao waliokuwa wakitokea Nairobi kwenda Dar es Salaam kwa shughuli za kidini.

Kamanda Mangu alisema lori hilo lililigonga basi hilo dogo baada ya basi hilo kusimama ili kutoa msaada kwa wanakwaya waliokuwa  kwenye basi lingine lililokuwa mbele ambalo liliacha njia na kupinduka upande wa kulia wa barabara hiyo kwa chanzo ambacho bado kujulikana.

“Basi hilo lilisimama na abiria waliteremka ili kutoa msaada kwa wenzao ambao basi lao lilikuwa limepinduka upande wa kulia wa barabara ukitokea Tanga. Wakati wakiendelea kufanya uokozi ghafla likaja lori lililokuwa linatoka Tanga kwenda Dar es Salaam likaligonga basi lile dogo lililokuwa limesimama.

“Wakati dereva wa lori anajaribu kulimiliki lori hilo ili litulie barabarani, ghafla alijikuta kigongana uso kwa uso na lori lingine ambalo lilikuwa likitokea Dar es Salaam kuelekea Arusha.
Tukio hilo limesababisha wanakwaya 11 ambao ni raia wa Kenya kufa papo hapo na wengine 25, kujeruhiwa vibaya,” alisema Kamanda Mangu.

Kamanda huyo alisema kutokana na ajali hiyo, magari yaliyokuwa yakisafiri kati ya Dar es alam na mikoa ya Kaskazini zikiwemo pia nchi jirani za Kenya na Uganda yalishindwa kupita katika neo hilo kutokana na malori hayo kufunga njia na hadi jana mchana jitihada za kuyaondoa malori hayo zilikuwa zinafanywa.

“Tunaendelea kutafuta ufumbuzi ili kuyaondoa malori hayo na magari yaweze kupita, tuna hakika wa kukamilisha kazi hiyo mchana huu,” alisema Kamanda Mangu.

Kuhusu marehemu waliokufa katika ajali hiyo, Kamanda Mangu alisema walipelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili huku majeruhi wakikimbizwa katika Hospitali ya Tumbi, Kibaha na wengine Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.

Taarifa tulizopata baadaye zilisema kwamba majeruhi waliofikishwa Kibaha nao walipelekwa Muhimbili baada ya kufanyiwa huduma za kwanza. Alisema dereva wa lori aliyeligonga basi hilo dogo la abiria anashikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi.

Wakati huo huo, habari kutoka Kenya, zilizopatikana jana zilisema Rais wa Kenya, Mwai Kibaki ameagiza ndege za nchi hiyo kuja Tanzania kuwabeba majeruhi na kuwakimbiza katika hopitali za Kenya kwa matibabu zaidi.

Hata hivyo habari hizo hazikueleza ni lini ndege hizo zitawasili nchini ili kuwachukua majeruhi hao.

No comments:

Post a Comment