.

.

.

.

Monday, February 18, 2013

MAONYESHO YA MAVAZI LONDON


Mheshimiwa Balozi Peter Kallaghe akiwa na mwanamuziki Freddy Macha aliyetumbuiza shughuli hii na gitaa lake.
- -
 Maonyesho maarufu ya mavazi  –London Fashion Week-  yaliyoanza rasmi Ijumaa iliyopita mjini London yameiweka ramani ya  Tanzania duniani. 
Shughuli hii muhimu kiuchumi na kisanaa inayoendelea  juma zima  na kuhusisha vituo vya kitamaduni na balozi 27  ina lengo la kutangaza vipaji vya wabunifu mavazi toka  nchi zisizojulikana  uwanja huu mahiri wa kimataifa unaosifika takriban miaka 30 sasa.
 “London Fashion Week”  ni moja ya maonyesho manne ulimwenguni yaliyoasisiwa rasmi kutukuza  ubunifu, ufundi na biashara  mwaka 1984.  Huendeshwa sambamba miji  ya New York, Milan na Paris kila mwezi Februari na Septemba.
Watanzania tulioingia  kwa dhamira ya “Swahili Flavour” (Ladha ya Kiswahili) tumefadhiliwa na  Ubalozi wa Tanzania London ukishirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB). Watayarishaji wa shughuli hii ni shirika la kitamaduni na elimu Uingereza- British Council lenye mahusiano ya kirafiki na nchi 100 duniani. “Maonyesho ya mavazi London ni fani ya hali ya juu na kibiashara ambapo waume kwa wanawake huwa pamoja wakibadilishana mapambo na visaidizi vyake,” anasema Julian Roberts, mbunifu mavazi wa British Council. 
Akiongea rasmi kwenye ufunguzi wa Ijumaa uliokuwa na vinywaji baridi na muziki wa Kiswahili, mke wa Balozi  Uingereza, Mama Joyce Kallaghe aliwasifu wabunifu mavazi wetu na kuwakabirisha wageni mbalimbali  waliohudhuria “kuzitembelea mbuga nzuri za Kitanzania kama watafurahishwa na mavazi na ladha yetu ya Kiswahili.”
 Wabunifu na washoni hao watatu ni Christine Mhando (  “Chichia London”),  Anna Lukindo ( “Anna Luks”) na Jacquleine Kibacha (“Heart 365”). Kibacha ambaye pia ni mtunzi wa mashairi huchanganya desturi za kijadi na kisasa kwa shanga shanga, manyoya ya ndege na mapambo yaliyotokana na sanaa za Wamasai. Miezi mitatu iliyopita kazi zake Kibacha zilipata tuzo maarufu la “Fashions Finest 2012.”
Akifafanua fani yake, Christine “Chichia” Mhando aliyehitimu chuo cha Usanii cha Kent mwaka 2002 alisema yeye huhamasisha vazi la Kanga, misemo na maneno ya Kiswahili mathalan “Tongoza”, “Ala Kumbe!” na “Zungumza” kama wajihi wa kazi hiyo.  Anna Luks aliyefuzu shahada ya mwanzo (BA) chuo cha Middlesex, alieleza azma  yake ni kumwonyesha mwanamke wa Kitanzania alivyo kupitia  mitindo kama “dunia pana” , “kaba roho” na “baibui.” Anna Luks huchanganya ushonaji wa mikono, kamba kamba na mavazi ya kisasa.  
 Naibu Balozi, Mheshimiwa Chabaka Kilumanga alisema maonyesho haya ya kimataifa yatakua nafasi kubwa kwa Tanzania kujitangaza kibiashara na ni sehemu mahsusi ya fahari ya utamaduni wetu. 
Wahusika wengine waliochangia  mafanikio ya shughuli  ni Mratibu Ubalozini, Bi Rose Kiondo; Afisa mwangalizi wa onyesho hilo, Samson Soboye na  Meneja  wa dhana  ya Swahili Flavour,  Mike Puplampu.
Habari zilizopatikana jana zilisema kwamba wabunifu mavazi wa Kitanzania wametajwa ndani ya kundi la washindi kumi bora. Ushindi huo unathibitisha dhahiri uwezo wa sanaa na ubunifu wetu ndani ya hulka ya mavazi ya kimataifa.
 Toka kulia, Mama Balozi- Joyce Kallaghe,  Anna Lukindo,  Mheshimiwa Balozi Peter Kallaghe,  Christine Mhando,  Naibu Balozi Chabaka Kilumanga na mkewe Irene. Picha na Urban Pulse


 Anna Luks, Mama Mhando na Chichia
 Mshoni Christine Mhando (Chichia London) akiongea na baadhi ya wageni
Moja ya vazi la kanga lililobuniwa na Chichia. Picha ya Urban Pulse
 Jacquiline Kibacha anayetumia jina la Heart 365. Picha na F. Macha
 Jacquiline Kibacha akipokea tuzo ya mapambo iitwayo “Fashions Finest 2012” mjini London mwezi Novemba mwaka jana
Moja ya ubunifu wa Jacquiline Kibacha uliohamasishwa na jadi ya Wamasai. 
Moja ya Ubunifu wa Anna Luks. Picha na Urban Pulse

No comments:

Post a Comment