.

.

.

.

Wednesday, February 20, 2013

ASKOFU SHAO ALIA NA SELIKALI


ASKOFU wa Kanisa Katoliki, Jimbo la Zanzibar, Augustino Shao na ndugu wa marehemu wa Padri Evarist Mushi wameitupia lawama Serikali kwa kuzembea kuwalinda viongozi wa dini hiyo waishio Zanzibar licha ya kupewa taarifa za viashiria vya hatari mara kwa mara.
Askofu Shao alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Zanzibar na ndugu wawili wa Padri Mushi walieleza hayo huko Moshi.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu alisema jana kwamba hawajapata malamamiko yaliyoelezwa na Askofu Shayo na kwamba kama Rais Jakaya Kikwete angeyapata asingeacha kuyashughulikia.

Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa naye alikanusha madai hayo akisema:
“... Hapa tulipo tuna kesi nyingi na kuna watu wanahojiwa. Sisi hatufanyi kazi kwa shinikizo la mtu, kama ni hivyo vipeperushi hata sisi tunavipata siyo wao tu. Sasa tutawakamataje wakati watu wenyewe hatuwajui?”

Hata hivyo, Askofu Shao alisema hawaridhishwi na utendaji kazi wa Polisi na kudai kwamba Wakristo wa madhehebu yote wanalengwa na mashambulio yanayofanywa na watu aliosema kuwa wanapata msaada kutoka nje.

“Niseme wazi tu, haturidhishwi na utendaji wa Serikali katika kutulinda. Tumemwandikia barua Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein na Rais Jakaya Kikwete tukiwaeleza vitisho tunavyopewa, lakini hatuoni hatua zikichukuliwa,” alisema Askofu Shao na kuongeza:

“Walipomshambulia Padri Ambrose Mkenda watu hao walileta ujumbe kwamba, tumeshawaweza Padri Ambrose na Sheikh Fadhil Soraga na bado tutaendelea. Vijana wetu wa kazi wameshamaliza mafunzo Somalia,” alinukuu moja ya kipeperushi huku akisema kuwa tatizo la Serikali ni kutokuwajibika.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Aboud Mohamed alikiri kupokea taarifa hizo za vitisho na kusema Serikali ina vyombo na taratibu zake katika kufanya kazi... “Sasa unataka Rais akamate wahalifu? Nadhani mtu sahihi wa kuzungumzia mambo haya atakuwa Kamishna wa Polisi. Ni kweli taarifa zimeletwa lakini nasi tulizipeleka kwenye vyombo vinavyohusika navyo ni Polisi.”

Askofu Shayo aliisifu Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akisema imejizatiti... “Bara wana nguvu, mtu akifanya kosa leo anakamatwa, lakini Zanzibar wanafanya kazi kwa kujuana.”

Askofu huyo alipinga kauli ya Serikali kuwa itahusisha taasisi za kimataifa kuwasaka wahusika wa mauaji akisema Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) likishirikiana na wananchi wanaweza kupata suluhu.

“Jeshi halijashindwa kumaliza uhalifu huu. Ukileta askari wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) watashindwa tu kwani hata Kiingereza hakitaeleweka. Bado watahitaji kupata msaada wa wananchi. Serikali inawajua wanaohusika, wanajua wanakokaa, tatizo ni uwajibikaji,” alisema Askofu Shao.

Hata hivyo, alisema kuwa hana ugomvi na Waislamu, bali anatofautiana na watu wote, wakiwamo Wakristo wanaotumia mgongo wa dini kufanya vurugu za kidini.
Askofu wa Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycap Kadinali Pengo alisema kuwa mauaji ya Padri Mushi yangeweza kuzuiliwa kama viongozi wa nchi wangesoma alama za nyakati.

Akizungumza na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) jana Kadinali Pengo alisema ni muhimu viongozi wa nchi kuchukua hatua na kuzuia yanayotokea na kuhusisha dini fulani.

Akimzungumzia marehemu Padri Mushi, Askofu Shao alisema: “Alikuja hapa Zanzibar tangu alipokuwa na miaka 18 akiwa anasoma elimu ya sekondari.

Mazishi yake

Askofu Shao alisema kuwa Ibada ya Mazishi ya Padri Mushi itafanyika Jumatano katika Parokia ya St. Joseph, Minara Miwili, Zanzibar na mwili wake utazikwa eneo la Kitope wanakozikwa viongozi wa kanisa.

No comments:

Post a Comment