.

.

.

.

Thursday, May 23, 2013

MACHAFUKO MTWARA


 Hali ya usalama mkoani Mtwara ni tete. Mtu mmoja anaaminika kufariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa kutokana na vurugu kubwa zilizozuka jana huko Mtwara baada ya kusomwa hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Madini na Nishati bungeni Dodoma jana.
Aidha, askari wanne wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), wamefariki dunia katika ajali wakitokea Nachingwea kwenda Mtwara ili kusaidia kutuliza vurugu hizo. Katika ajali hiyo, askari 20 walijeruhiwa, wengi wao vibaya na saba walinusurika.
Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Ligula, Dk Mohamed Kodi alithibitisha kupokea maiti moja na kuomba apewe muda kutaja idadi ya majeruhi.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Linus Sinzumwa alidai kwamba hakuna mtu aliyefariki dunia wala majeruhi. Alisema watu 45 wamekamatwa.
Milio ya risasi za moto na mabomu ya machozi vilisikika kila kona na hasa Mitaa ya Mdenga, Magomeni na Shengena Mjini Mtwara ambako hali ilikuwa mbaya kutokana na kuwapo kwa mapambano kati ya polisi na vijana.
Vurugu hizo zilitokana na hatua ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kusisitiza kuwa bomba la gesi kutoka Mtwara na kuja Dar es Salaam litajengwa, jambo lingine linalodaiwa kusababisha ghasia hizo ni hatua ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kutokurusha moja kwa moja matangazo ya Bunge hivyo kuwakosesha wananchi fursa ya kusikiliza bajeti hiyo.
Akizungumzia kukosekana kwa matangazo hayo ya televisheni, Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Clement Mshana alisema kukatika kwa matangazo hayo kulitokana na tatizo la satelaiti katika mji huo na Musoma.
Hata hivyo, wakazi wa Mtwara waliokuwa na ving’amuzi walipata fursa ya kuangalia matangazo hayo.
Pia vurugu hizo zilichangiwa na vipeperushi vilivyosambazwa na watu wasiojulikana wakitaka watu kuacha kufanya shughuli zozote na kukaa nyumbani ili kufahamu hatima ya mradi wa usafirishaji wa gesi kutoka Msimbati hadi Dar es Salaam kwa njia ya bomba.
Katika vurugu hizo zilizozagaa zaidi maeneo ya Mikindani na Magomeni, wananchi pia waliharibu Daraja la Mikindani linalounganisha Mikoa ya Dar es Salaam, Lindi na Mtwara.
Tangu asubuhi kama ilivyokuwa Mei, 17 mwaka huu, Mji wa Mtwara ulikuwa kimya na huduma nyingi za kijamii zilisimama ikiwamo usafiri wa pikipiki, daladala, mabasi maduka na masoko.

No comments:

Post a Comment