.

.

.

.

Monday, May 13, 2013

MH. RAIS DKT JAKAYA KIKWETE ATEUA MABALOZI WAPYA


 Rais Jakaya Kikwete
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, amefanya uteuzi wa Mabalozi Wapya kujaza nafasi zilizo wazi na kuanzisha Ofisi za Ubalozi nchini Uholanzi na Comoro.  Aidha Mheshimiwa Rais amefanya uhamisho wa Balozi kutoka kwenye kituo kimoja.

Mabalozi wateule na aliyehamishwa kituo ni kama ifuatavyo:-

Bw. Wilson M. K. Masilingi;
Ameteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi. Bw. Masilingi ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kituo cha Mikutano cha Kimataifa, Arusha, (AICC) na aliwahi kuwa Mbunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kati ya mwaka 1995 – 2010.  Aidha, katika kipindi cha mwaka 1998 – 2005 alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais mwenye dhamana ya masuala ya Utawala Bora.

Bw. Chabaka Faraji Ali Kilumanga, ameteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Comoro. Hadi uteuzi huu unafanyika, Bw. Kilumanga alikuwa Balozi Mdogo katika ofisi ya Ubalozi nchini Uingereza.

Bw. Modest Jonathan Mero, ameteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa, Geneva.  Kabla ya uteuzi Bw. Mero alikuwa Afisa wa Mambo ya Nje Mwandamizi kwenye Ubalozi wa Tanzania katika Ofisi za Umoja wa Mataifa, New York.

Kadhalika, Mheshimiwa Rais amemhamisha Balozi Philip Sang’ka Marmo kutoka Ubalozi wa Jamhuri ya Watu wa China na kwenda Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani.
 


------MWISH0-----




(John M. Haule)


KATIBU MKUU,


WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA,

DAR ES SALAAM.

12 MEI, 2013

No comments:

Post a Comment