.

.

.

.

Wednesday, April 29, 2015

MZEE YUSSUF KUIMBA NA DIAMOND PLATNUMZ


KIONGOZI wa kikundi cha muziki wa taarab cha Jahazi, Mzee Yussuf, amesema yuko tayari kuimba wimbo wa miondoko hiyo kwa kushirikiana na nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Naseeb Abdul 'Diamond'.

Mzee ameelezea msimamo wake huo baada ya Diamond kukaririwa na vyombo vya habari wiki iliyopita akisema kuwa, anataka kuimba wimbo wa taarab kwa kushirikiana na Mzee Yussuf.

"Nimepata taarifa kwamba Diamond anataka kuimba taarab na mimi. Mi nasema nipo tayari kufanya hivyo wakati wowote,"alisema Mzee, ambaye pia anajulikana kwa jina la 'Mfalme'.

Nyota huyo wa taarab alisema kwa kipindi cha miaka 11, ambacho amekuwa akijihusisha na muziki huo, amefanya mambo mengi katika kuutangaza ndani na nje ya nchi na pia kuibua vipaji vya wasanii mbalimbali.

"Katika kipindi cha miaka 11 iliyopita, nimefanya mambo mengi na kuwatoa wasanii wengi mpaka leo hii naitwa mfalme,"alisema Mzee, ambaye ameoa wake wawili, akiwemo Leila Rashid, ambaye ni miongoni mwa waimbaji nyota wa Jahazi.

"Leo hii hakuna asiyemfahamu Isha Mashauzi, Thabiti Abdul, Ally J na wengineo. Wote hao ni matunda yangu,"alisema msanii huyo wa zamani wa vikundi vya East African Melody na Zanzibar Stars.

Mzee alisema si kweli kwamba alipanga kustaafu muziki huo mwaka huu, kama alivyonukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari. Alisema atafanya hivyo baada ya kuuweka muziki wa taarab kwenye chati ya juu.

Alisema alichomaanisha ni kwamba akitoa wimbo mpya, ndio utakuwa wa mwisho na hatoimba tena zaidi ya kuendelea kuwa mtunzi na shughuli zingine za nyuma ya muziki.

“Nilisema nitakapoimba wimbo mwingine, utakuwa wa mwisho sitaki tena kuimba, nimeshachoka kuimba,” alisema Mzee.

Alidai kuwa alianza muziki tangu mwaka 1997, lakini alianza kuimba mwaka 2004 na muda huo alikuwa akitunga nyimbo za watu wengine.

“Mimi kwenye bendi sifanyi kitu kimoja, natengeneza nyimbo za watu wote, napiga vinanda,” alisema.

Kwa upande wake, Diamond alisema anafikiria kujitosa katika muziki wa taarab baada ya kupata mafanikio makubwa katika muziki wa taarab.

Diamond alisema amefikia uamuzi huo kutokana na kuvutiwa na muziki huo wa taarab, ambao pia ni maarufu kwa jina la mipasho.

Kauli hiyo ya Diamond ilikuja siku chache baada ya kuibuka na kibao kipya cha miondoko ya mduara, akimshirikisha malkia wa taarab nchini, Khadija Kopa.

Mshindi huyo wa tuzo mbalimbali za muziki za Kilimanjaro amesema, anajua uamuzi wake huo utawashangaza mashabiki wengi, lakini ni jambo la kawaida kwa msanii.

Diamond alisema hadi sasa anaamini hana mpinzani katika muziki wa kizazi kipya na hakuna msanii anayeweza kufikia kiwango chake hapa nchini.

“Najua watu watanishangaa na kuniona mtu wa ajabu, lakini nimefanya hivyo kwa sababu sina mpinzani katika muziki wa kizazi kipya,”alisema.

Diamond alisema ameamua kupiga miondoko tofauti ya muziki kutokana na kipaji alichonacho katika fani hiyo, ambayo imempatia umaarufu mkubwa kimataifa na kumwezesha kutembelea nchi kadhaa za Ulaya.

Kutokana na kipaji chake hicho, Diamond alisema hakuna kitu anachoshindwa kukifanya katika muziki.

“Bado sijaanza rasmi kupiga muziki wa taarab, ninachokifanya kwa sasa ni kufanya tathmini ya soko lake ili kuona kama unaweza kuniletea mafanikio kama ilivyo kwa muziki wa bongo fleva,”alisema msanii huyo.

“Naweza kufanya kila aina ya muziki kwa sababu nina kipaji cha kuimba nyimbo aina zote, hivyo endapo nitafikia muafaka, naweza kufanya kitu hicho ingawa mashabiki wangu watashtuka sana,” alisema.

Diamond alikiri kuwa, muziki wa kizazi kipya umemfanya ajulikane sehemu nyingi duniani, ikiwa ni pamoja na kupata manufaa mbalimbali kimaisha kwa kuishi kwenye nyumba nzuri na kumiliki magari ya kifahari.

Msanii huyo mwenye haiba ya kuvutia alisema, kwake muziki ni kazi kama zilivyo kazi zingine hivyo amekuwa akifanya kazi zake kwa malengo.

Alisema siri kubwa ya muziki wake kuwateka mashabiki wengi ndani na nje ya nchi ni kufanyakazi zake kwa kujituma na pia kujiwekea malengo.

"Sifanyi muziki kwa ajili ya kujifurahisha, kutafuta pesa na kuwaacha mashabiki wangu wabaki na kiu ya burudani,”alisema Diamond.

“Ninapofanya muziki nahakikisha kuwa, nakata kiu ya mashabiki wangu kwa kuwapa burudani wanayoihitaji,”aliongeza.

Katika kufanikisha hilo, Diamond alisema amekuwa na utaratibu wa kushirikiana na watu mbali mbali kwa vile anaamini sio rahisi kuweza kufanya kila kitu peke yake.

Alisema miongoni mwa watu, ambao wamekuwa wakimpa ushirikiano mkubwa katika kazi zake ni wacheza shoo kwa vile wamekuwa wakibuni vionjo vipya kila kukicha.

"Siwezi kuwa na ubahili ninapofanya kazi na hili ndilo lililonifanya nizidi kusonga mbele katika kazi ya muziki. Ili upate ni lazima utoe na ili uwafurahishe mashabiki wako ni lazima uzingatie kanuni hizo,”alisema.

No comments:

Post a Comment