.

.

.

.

Tuesday, September 30, 2008

CHADEMA NA SAKATA LA "WANGWE"




KIFO cha Mbunge wa Tarime, Chacha Wangwe kinazidi kuibua mengi baada ya mke wake wa kati Dotto Mohamed kukana maelezo ya mke mdogo Mariam Wangwe kwamba Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeitelekeza familia.
Akizungumza jana, Dotto alisema kauli ya Mariam ni nzito mno kuitoa sasa kwani anaamini matukio yanayoendelea baada ya kutokea msiba huo, ndiyo yanayoweka pazia la mawasiliano kati ya Chadema na familia ya Marehemu.
"Sijaisoma taarifa yote ila mtoto wangu ameniletea gazeti ambalo bado ninalo. Mimi ninashindwa kufikiria wala kuwaza kuanza kukilaumu Chama kwamba kimetutelekeza kwani ni mapema mno kufanya hivyo na wote bado tuko kwenye majonzi," alisema Dotto na kuongeza:
Nasema nashindwa kukilaumu chama kwa sababu tangu kutokea kwa msiba huo hakuna aliyetulia, familia bado ina majonzi, chama chenyewe bado kinalia na hata jamii inaendelea kumlilia Wangwe nasema familia yangu bado ina imani na chama na hatuwezi kukilaumu sasa," alisema.
Dotto alisema anaamini Chadema inaongozwa na watu wenye busara hivyo hawezi kuinenea mabaya kabla ya kuridhika kwamba viongozi hao wameanza kupingana na busara hiyo.
"Ninihitaji muda kupima hekima ya chama kabla sijakihukumu kwani kinyume chake nitakuwa sijakitendei haki," alisema.
Alisema mpaka sasa bado anaamini kuwa Chadema iko sambamba na familia ya marehemu Wangwe kwani hata kwenye arobaini iliyofanyika kijijini Komakorere chama hicho kilituma wawakilishi.
Mke huyu wa pili wa Chacha Wangwe anaishi jijini Mwanza na jana alikuja jijini Dar es Salaam kuwachukua watoto wake wawili waliokuwa wakiishi na Mariam, mke mdogo wa Wangwe.
Jana Dotto alisema kuwa katika safari yake hiyo pia amepanga kukutana na Mariam na kuzungumza naye ili ajue kiini cha shutuma zake kwa Chadema.
"Kuja kwangu Dar es Salaam ni pamoja na kuwachukua wanangu wawili ambao wamekuwa wakiishi na Mariam; katika ujio huo tutakaa tuzungumze anieleze kwa nini ameamua kuzungumza maneno hayo sasa,".
Alisema hata kama Mariam atafanikiwa kumshawishi aamini maneno yake, bado atahitaji muda kukubaliana naye kwani anaamni kuwa bado ni mapema mno kutoa shutuma hizo.
"Sisi bado tuna imani na Chama na hatuwezi kujua chama kinatuwazia nini hivyo narudia: ni mapema mno kutoa shutuma hizo kwani wote bado tuko kwenye majonzi," alisisitiza.
Akizungumzia kauli ya Dotto, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema ndiyo aliyotarajia kusikia kutoka kwa familia ya marehemu Wangwe.
"Nafikiri kauli hiyo ndiyo niliyotarajia kutoka kwa familia ya Wangwe ninayemfahamu kwa sababu kama utakumbuka tangu mwanzo wa msiba, sisi (CHADEMA) tulikuwa tukisakamwa sana lakini tulikaa kimya kwa busara ili tusimkamate mchawi asiyetuhusu," alisema.
Dk Slaa ambaye alisisitiza kwamba hamfahamu Mariam kama mke wa marehemu Wangwe, alisema anasikitishwa na kauli yake ambayo anaamini kuwa imelenga kukichafua chama.
Hiki anacholalamikia kwamba Chadema hawakuhudhiria arobaini ya mume wake, nashindwa kuelewa. Kumbuka mimi nina miaka 60 na tangu nianze kufahamu arobaini, najua zinafanyika mahala alikozikwa marehemu.
Wangwe alizikwa Komakerere na arobaini yake ilifanyika huko na Chadema tulituma mwakilishi. Hii arobaini aliyoifanya Mariam na Profesa Wangwe Dar es Salaam hatukuijua wala wao hawakutaka Chadema iijue," alisema.
Akifafanua alisema ingawa Mariam alitoa taarifa ya arobaini aliyoifanya Dar es Salaam, waalikwa katika taarifa hiyo ni wabunge kwa majina yao na sio Chadema kama taasisi.
Alisema pamoja na kasoro hiyo wabunge wa Chadema Suzan Lyimo na Grace Kihwelu walihudhuria kwa kofia zao lakini waliwakilisha chama kwa salamu ambazo zilisomwa na Lyimo katika hafla hiyo.
"Mimi Dk Slaa nilialikwa kwa ubunge wangu na sio ukatibu mkuu wa Chadema na Mbowe alialikwa kwa jina lake na sio uenyekiti wa Chadema vivyo hivyo wabunge wengine. Sasa Chadema inapolaumiwa tunashindwa kuelewa.

No comments:

Post a Comment