.

.

.

.

Thursday, October 09, 2008

MWANAMKE AFANYIWA UNYAMA

Mwanamke mmoja amefanyiwa unyama wa kutisha na mumewe baada ya kufyekwa viganja vyote vya mikono kutokana na kile kinachodaiwa kuwa ni baada ya yeye kukataa kumpa maraha ya unyumba. Mwanamama huyo aliyetajwa kwa jina la Somoe Mcharaganya, 32 (pichani mbele), ambaye ni mkazi wa Mkuranga mkoani Pwani, hivi sasa yuko hoi, pale katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako madaktari wangali wakihaha katika kunusuru maisha yake. Akisimulia kwa taabu juu ya mkasa huo, Bi. Somoe aliyelazwa katika wodi mojawapo ya Taasisi ya Mifupa Muhimbili, MOI, amesema amekutwa na mkasa huo hivi karibuni, mishale ya saa 1:00 usiku. Akadai kuwa chanzo cha yote hayo kumfika ni yeye kutojisikia vizuri kimwili na hivyo kumkatalia unyumba mumewe huyo. Akasema siku hiyo ya tukio, yeye alikuwa akijisikia vibaya kufuatia kipigo cha awali alichopewa na mumewe aliyemtaja kwa jina Hassan Nyamnyigani, ikiwa ni siku moja tu iliyopita baada ya mumewe huyo kumtuhumu kuwa amewasiliana kwa simu na wanaume aliowahisi kuwa ni hawara zake. ``Nilikuwa nimeomba simu kwa jirani ili niwasiliane na ndugu zangu... aliponikuta nikifanya hivyo, akanipiga sana na kunifanya nijisikie vibaya,`` akasema. Akasema siku ya pili yake, wakati mumewe alipomuomba walale na kupeana maraha, yeye alikataa kutokana na ukweli kuwa bado alikuwa akiuguza majeraha ya kipigo cha jana yake. ``Nikamwambia mwezangu kuwa sijisikii vizuri... ndipo alipojaribu kunilazimisha bila mafanikio na hapo nd\'o akapandwa hasira na kuanza kunipiga kwa panga,`` akasema. Akasema alikuwa akimpiga kichwani kwa panga, hivyo yeye akawa akijiziba kichwa kwa mikono ili asiuawe na ndipo viganja vyote vikakatika. ``Nilipiga sana kelele... mwenzangu alipoona damu zikinivuja na pia aliposikia milio ya vifupa vya mkono, akadhani ameshanipasua fuvu la kichwa, hivyo akatoka na kukimbia,`` akasema Somoe ambaye anasema baada ya hapo, aliokolewa na majirani ambao walimuwahisha katika hospitalini. Afisa Uhusiano wa MOI, Bw. Almas Jumaa, amesema mgonjwa huyo alifikishwa kwao akiwa hoi, akitokea katika Hospitali ya Mkuranga na kwamba sasa ana nafuu kulinganisha na wakati akifikishwa hapo. Mwandishi hakuweza kumpata Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Absolom Mwakyoma ili azungumzie tukio hilo. Hata hivyo, inaelezwa kuwa mwanaume aliyetenda unyama huo alilala mbele na bado hajakamatwa.

No comments:

Post a Comment