.
.
Monday, October 20, 2008
RASILIMALI KUZUA UTATA
CHAMA cha Wananchi (CUF), kimesema suala la mafuta na gesi asilia si la Muungano na kumtaka Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Abeid Karume, kuanzisha wizara maalumu ya mafuta na gesi asilia.
Kauli hiyo ya CUF imetolewa jana visiwani Zanzibar na Katibu Mkuu wa chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Kibanda Maiti.
Mbali na kumtaka Karume kuunda wizara hiyo, pia wametaka kuwepo kwa Shirika la Maendeleo ya Mafuta Zanzibar, ili liweze kutoa vibali vya uchimbaji wa mafuta na gesi katika vitalu namba 9, 10, 11 na 12 vilivyopo katika ukanda wa bahari kuu ya visiwa vya Unguja na Pemba .
Maalim Seif, ameilaumu Serikali ya Muungano kwa kijinufaisha peke yake katika suala hilo, kwa kisingizio kuwa Zanzibar haiwezi kuchimba gesi na mafuta kwa kuwa suala hilo ni la muungano.
Alisema Serikali ya Muungano imemzuia mwekezaji kutoka nchi za Falme za Kiarabu kujenga kiwanda cha kusafisha mafuta kwa kisingizio cha kuchafua mazingira.
Alisema badala yake viongozi wa Serikali ya Muungano walimshawishi mwekezaji huyo kujenga Tanzania Bara, kwa madai kuwa hakiwezi kuchafua mazingira ya Bara, kwa kuwa kuna eneo kubwa.
Maalim Seif, alisema baada ya vikwazo hivyo aliwasiliana na wawekezaji hao ambao walisema bado wana nia ya kuwekeza lakini sasa watalazimika kupitia Serikali ya Muungano.
Alisema aliwaambia wawekezaji hao kuwa Wazanzibari wataupinga kwa nguvu zote uwekezaji wa kupitia muungano ila watauunga mkono uwekezaji kupitia Serikali ya Zanzibar.
Alisema kutokana na hali hiyo, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imenyimwa fursa ya kujiendeleza kiuchumi pamoja na vijana wengi wa Zanzibar kupata ajira.
“Huu ni mkakati wa Serikali ya Muungano kuhakikisha kuwa suala la mafuta na gesi asilia linaendelea kuwa la muungano,” alisema katibu mkuu huyo.
Katibu mkuu huyo, alisema anayo taarifa kuwa Serikali ya Muungano inaandaa muswada, ili sheria ya uundwaji wa Shirika la Maendeleo la Mafuta Tanzania (TPDC) irekebishwe, kwa lengo la kuliwezesha shirika hilo liwe na muungano na kufanya kazi hadi Zanzibar.
“Mkakati huo umekuja baada ya kubainika kuwa Zanzibar kuna mafuta mengi hasa katika mwambao wa Zanzibar, ambako kumegundulika block 3 namba 9 hadi 12, ambazo zinaonyesha Zanzibar kuna mafuta, hasa katika mwambao wa Pemba.
“Msimamo wa CUF ni kwamba suala la mafuta na gesi asilia ni mali ya Zanzibar… upo ushahidi wa kutosha mafuta na gesi asilia vimeingizwa kwenye muungano kwa ubabe, wakati huo Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar alikuwa Abubakar Hamisi Bakari.
“Baada ya suala hilo kupitishwa na Bunge, Abubakar alikwenda kulalamika kwa Nyerere (hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere), lakini hakuna lolote lililofanyika mpaka sasa,” alisema katibu mkuu huyo.
Maalim Seif, alisisitiza kuwa ni busara suala la mafuta likabakia kuwa mali ya Zanzibar, kwa sababu Wazanzibari wengi hawapendi kuwa ya muungano, hivyo ni lazima kuepusha matatizo kama yale yanayotokea nchini Nigeria, ambapo kumekuwa na ugomvi wa mafuta.
“Tumeona nchi nyingi zikiwemo nchi za Ghuba zilikuwa maskini, lakini baada ya kuchimbwa mafuta katika nchi zao, sasa wameweza kupata utajiri na kuondokana na umaskini … haya matatizo ya kulipia kodi naamini kwetu yataondoka ya kulipia watoto elimu, afya na huduma nyingine muhimu,” alisema.
Alisema mbali na suala la mafuta, imegundulika kuwa Zanzibar ni nchi ya pili duniani kwa kuwa na gesi nyingi, ikiongozwa na nchini ya Qatar.
Aidha, alisema msimamo wa Wazanzibari hadi sasa ni kuwa bahari kuu yote na inayopakana nayo ni mali ya Zanzibar na rasilimali zake, ikiwa pamoja na kumiliki kilomita 50,000 kutoka ufukweni mwa bahari.
“Eneo lote la mashariki ya Zanzibar ni eneo la Zanzibar, lakini Serikali ya Muungano inafanya jitihada ili masuala ya bahari yawe ya muungano,” alisema.
Wakati huo huo, Maalim Seif, alisisitiza kuwa Zanzibar ni nchi, kwani ina sifa zote zinazotakiwa, ikiwa ni pamoja na kuwa na ukanda maalumu kiuchumi upatao kilomita 200.
Katika mkutano huo, watu wengi walionekana kuvaa fulana zilizoandikwa ‘Zanzibar ni nchi’ na nyingine ‘mwisho wa ufisadi 2010’ na nyingine zilikuwa zikiendelea kuuzwa katika viwanja hivyo kwa bei ya sh 5,000.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment