WIKI moja kabla ya hatima ya watuhumiwa wa ufisadi kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) kujulikana, wafadhili kutoka nchi 14 kupitia Benki ya Dunia, wametangaza kutoa mabilioni ya fedha kwa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete. Pamoja na msaada huo uliotangazwa jana, wafadhili hao ambao walisita awali kuutoa kutokana na tuhuma za ufisadi, walionya kuwa msaada zaidi mwakani utategemea namna uamuzi juu ya ufisadi wa EPA utakavyotolewa. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na ofisi ya Benki ya Dunia nchini, msaada huo wa maendeleo ambao ni mkopo wa dola milioni 160 (zaidi ya sh. bilioni 160) ulioridhiwa juzi na Bodi ya Utendaji ya Benki hiyo, unalenga kutumika kusaidia bajeti hasa katika miradi ya Mkakati wa Kuinua Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA), uliozuiwa kwa miezi sita kutokana na kadhia ya EPA. "Mkopo huo ulicheleweshwa kwa miezi sita baada ya kuibuka kwa kashfa ya ufisadi kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) iliyoko Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ili kuipa muda Serikali ichukue hatua za dhati kurekebisha hali hiyo. "Katika kufikia uamuzi huu, kwanza Shirika la Fedha Duniani (IMF) lilifanya tathmini ya kujihakikishia usalama kwenye BoT hasa uwezo wake wa udhibiti na usimamizi," ilisema taarifa hiyo. Ikielezea sababu zaidi zilizowafanya wafadhili hao kuvunja uamuzi wao wa awali wa kususia kusaidia bajeti hiyo, taarifa hiyo ilisema: "Ili kuendelea kupokea misaada ya hali ya juu kutoka Benki ya Dunia, vigezo vinavyoangaliwa ni pamoja na harakati za kupambana na rushwa, kuimarishwa kwa uwazi na utawala bora na udhibiti wa matumizi ya fedha hasa katika taasisi za umma na mikataba mikubwa." Hata hivyo pamoja na Tanzania kupewa mkopo huo utakaotakiwa kulipwa katika kipindi cha miaka 40, huku Serikali ikipewa kipindi cha huruma cha miaka 10 iwapo itashindwa kulipa katika miaka hiyo ya awali, Benki ya Dunia imempa Rais Kikwete na Serikali yake, mtihani mgumu. Taarifa ya Benki hiyo ilisema uamuzi kuhusu watuhumiwa wa EPA ambao Serikali itautoa, utatumika kuitathimini mwakani iwapo itakidhi kupewa tena msaada kwenye bajeti.
No comments:
Post a Comment