LEO Wakristo kote duniani wanasherehekea Sikukuu ya Krismasi, ambayo ni kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo zaidi ya miaka 2000 iliyopita.
Ni sherehe ambazo huadhimishwa kila mwaka inapofika tarehe kama hii ya leo na pia huashiria kumalizika kwa mwaka na kuanza mwaka mpya.
Kwa wengine, kipindi hiki cha Sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya ni kipindi cha mapumziko.
Ni vyema kutumia muda huu wa mapumziko kupima mafanikio ya mwaka uliopita na kupanga ya mwaka ujao utakavyokuwa.
Kwa Watanzania, katika kuadhimisha siku hii ya leo, shamrashamra zinapaswa kujikita kwenye changamoto nyingi zinazolikabili taifa kwa sasa, likiwemo suala la ufisadi, mauaji ya ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi (maalbino), wanaouawa kwa imani za kishirikina.
Kikubwa ambacho Watanzania tunapaswa kukizingatia katika furaha zetu leo ni kudumisha amani na utulivu ambavyo vimelifikisha taifa hapa lilipo.
Kila aliyebarikiwa na Mola kuiona siku hii ya leo, hana budi amshukuru na afanye shughuli zake kwa utulivu ili kuepuka migogoro ya aina yoyote ile.
Kwa Wakristo wote duniani, Krismasi maana yake ni kuzaliwa upya na Kristo Mfalme.
Familia ziende nyumba za ibada kumshukuru Mungu kwa yote aliyowatendea mwaka mzima na kumwomba awavushe kuuona mwaka mpya wa 2009 kwa heri na amani.
Kama kawaida, waumini wataingia makanisani kuabudu na kushukuru na wale ambao hawataingia, watumie muda wa mapumziko kufanya vitu vingine vyenye sababu anuai kuonyesha furaha yao.
Hata hivyo tungependa kuwaasa wananchi kutotumia vibaya siku ya Krismasi kufanya mambo ya upuuzi ambayo yataangamiza familia au wao wenyewe na kulitia hasara taifa.
No comments:
Post a Comment