.

.

.

.

Wednesday, February 04, 2009

CCM NA CUF

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimemtaka Katibu Mkuu wa CUF, Seif Sharif Hamad, kumwomba radhi Rais Jakaya Kikwete, kutokana na kauli na matamshi yasiyo ya kistaarabu.Pia CCM Zanzibar imevitaka vyombo vya Dola kufuatilia kwa makini kauli zinazotolewa na viongozi wa CUF ambazo zinalenga kuleta vurugu na kuhatarisha amani na utulivu. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Idara ya Itikadi na Uenezi ya CCM Zanzibar ikiwa imesainiwa na Katibu wa Kamati Maalumu ya NEC Zanzibar, Vuai Ali Vuai, kauli zilizotolewa na viongozi wa CUF katika mkutano wa hadhara wiki iliyopita, zinakwenda kinyume na maadili ya Watanzania kwa kutukana viongozi wa kitaifa hadharani. Vuai alisema Katibu Mkuu wa CUF Seif Sharif Hamad alitoa matamshi ya hatari akimtaka Rais Kikwete 'akome' kuingilia masuala ya kisiasa ya Zanzibar.Aidha, aliwataka wafuasi wa CUF kujiandaa na uchaguzi mkuu mwakani na mdogo wa jimbo la Magogoni, bila kusubiri taarifa ya mtu yeyote. Katika mkutano huo, pia Seif alisema yeye ndiye anayeijua Zanzibar na si Kikwete ambaye alikuja visiwani hapa kama Ofisa Mdogo wa Makao Makuu ya CCM Kisiwandui. ”Ni kauli mbaya ya kumwambia Rais wa nchi akome … asiwagombanishe wananchi wa Zanzibar na hana ubavu wa kulinda Mapinduzi ya Zanzibar kwa sababu si Mzanzibari,” alisema Vuai. Akifafanua, Vuai alisema Rais Kikwete ni Kiongozi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na pia Mwenyekiti wa CCM iliyotokana na ASP na TANU, hivyo kulinda Uhuru na Mapinduzi ya Zanzibar ni jukumu lake kisheria na kikatiba.Hivi karibuni, CUF imekuwa ikimshutumu Rais Kikwete kwamba alitoa matamshi ya kuviza demokrasia ya vyama vingi nchini wakati wa ziara yake Pemba mwezi uliopita.


No comments:

Post a Comment