WAKATI serikali ikiendelea na mchakato wa zabuni ya vitambulisho vya uraia ya Sh222 bilioni, imebainika kwamba kiasi hicho cha fedha ni kikubwa mno na kama wangemtumia Mpigachapa wa Serikali kazi hiyo ingetumia Sh95 bilioni tu.
Habari zilizopatikana zinaeleza kwamba, ingawa mpigachapa wa serikali alishaomba zabuni hiyo kufanya kazi hiyo, lakini hajachaguliwa bila ya sababu maalumu.
Siri hiyo ilifichuka juzi wakati Kamati ya Bunge ya Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali (Miscellaneous Amendments) ilipotembelea ofisi ya Mpigachapa Mkuu kujionea utendaji kazi ikiongozwa na Kaimu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Benson Mpesya ambaye ni Mbunge wa Mbeya mjini kupitia CCM na kugundua kuwa ofisi hiyo ya serikali ina uwezo wa kufanya hiyo kazi kwa bei nafuu zaidi.
Mbunge wa Moshi mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Philimon Ndesamburo ambaye ni mjumbe wa kamati hiyo aliiambia Mwananchi Jumapili jana kuwa serikali, itoe sababu za kuikatalia Ofisi ya Mpiga Chapa Mkuu wake, kuandaa vitambulisho vya uraia kwa gharama ya Sh95 bilioni badala yake kung'ang'ania zabuni itakayogharimu Sh222 bilioni.
Akifafanua hoja yake mbunge huyo, alisema akiwa kwenye ziara hiyo, alimuuliza Mpigachapa Mkuu wa Serikali, Cassian Chibogoyo, kama Ofisi yake inao uwezo wa kuchapa vitambulisho vya taifa na aliwajibu wajumbe wa Kamati ya Bunge kwamba, ofisi yake inaweza kutengeneza vitambulisho hivyo kama itapatiwa fedha.
No comments:
Post a Comment