.

.

.

.

Tuesday, March 24, 2009

HOTELI ZA KITALII BAGAMOYO ZATEKETEA KWA MOTO


MOTO mkubwa uliokuwa ukipeperushwa kwa upepo, jana asubuhi uliziteketeza kwa moto hoteli kubwa tatu za kitalii zilizojengwa katika ufukwe wa Bahari ya Hindi, wilayani Bagamoyo.
Tukio hilo la kwanza la aina yake lilizikumba hoteli maarufu za Paradise Holiday Resort, Oceanic Bay na Livingstone, zote zikiwa ni zenye hadhi ya nyota tatu zilizokuwa zimeezekwa kwa makuti.
Moto huo unaoaminika kuanzia katika jiko la Hoteli ya Paradise kutokana na cheche ya moto iliyotokana na hitilafu ya umma, ulizuka majira ya saa 4:30 kabla ya kudaka paa na kuanza kusambaa katika majengo tofauti ya hoteli hiyo na hoteli za jirani, ukiifikia kwanza Hoteli ya Oceanic na kisha kuiunguza Livingstone.
Ofisa moja wa juu wa Hoteli ya Paradise inayoongoza kwa mikutano, semina na warsha, aliyezungumza na mwandishi wa habari hizi alisema, hesabu za haraka haraka zinaonyesha kuwa, hasara iliyotokana na ajali hiyo ya moto ambao ulizuka wakati baadhi ya wateja wa hoteli hizo wakiwa vikaoni, vyumbani na ufukweni, inaweza kuwa zaidi ya shilingi bilioni 20.
Mbali ya kuharibu majengo mbalimbali ya hoteli hizo ambazo zimejizolea umaarufu mkubwa kwa wateja kutoka ndani na nje ya nchi, moto huo uliyateketeza magari sita ya wateja yaliyokuwa yameegeshwa katika maeneo ya hoteli hizo, mawili kati yake yakiwa ni mali ya serikali.
Watu walioshuhudia moto huo wanasema ingawa hakuna taarifa za watu kujeruhiwa au kupoteza maisha katika ajali hiyo, ulipoanza kusambaa, kelele za vilio vya watu waliokuwa wakihangaika kunusuru mali na vifaa vyao zilikuwa zikisikika kutoka maeneo mbalimbali ya hoteli hizo na jirani.

No comments:

Post a Comment