.

.

.

.

Wednesday, March 25, 2009

YANGA BINGWA

MABAO mawili yaliyofungwa na Juma Kaseja na Mike Barasa yameweza kuipa Yanga ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuifunga Toto Afrika ya Mwanza katika mchezo wa Ligi hiyo uliofanyika katika Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza jana.
Yanga iliuanza mchezo huo kwa kasi na kufanikiwa kupata penati katika dakika ya 19 baada ya beki Ramadhan Hassan kumfanyia madhambi Nurdin Bakari ndani ya eneo la hatari. Hata hivyo Nurdin alipiga na kukosa penati hiyo.

Katika kile kilichoonekana kama rekodi ya mchezo wa Ligi Kuu, Juma Kaseja aliipatia Yanga bao la kuongoza katika dakika ya 22 baada ya kuanzisha mpira uliokwenda moja kwa moja wavuni baada ya kuguswa kidogo na kipa wa Toto.Kuingia kwa bao hilo kuliwafanya Toto kucheza kwa kujituma zaidi na kuweza kusawazisha bao hilo katika dakika ya 29 lililofungwa na Hussein Swed aliyeonekana kuisumbua vilivyo ngome ya Yanga.Kuingia kwa bao hilo, kuliiamsha safu ya ushambuliaji ya Yanga iliyojitahidi kulishambulia lango la Toto na kufanikiwa kupata bao katika dakika ya 32 lililofungwa kwa njia ya mpira wa adhabu na Mike Barasa. Mpaka mapumziko Yanga ilikuwa mbele kwa mabao 2-1.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku kila timu ikijitahidi kupata bao, lakini beki wa Yanga Fred Mbuna nusura aipe bao Toto katika dakika ya 63 baada ya kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari na kuipa timu hiyo ya Mwanza penati.Hata hivyo penati hiyo iliyopigwa na Rashid Roshwa ilipanguliwa na Kaseja na kuamsha shamrashamra kutoka kwa mashabiki wa Yanga waliojitokeza katika Uwanja wa CCM Kirumba.Mpaka mwisho wa mchezo Yanga ilitoka kifua mbele kwa ushindi wa mabao 2-1 na kufikisha pointi 46 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote.

No comments:

Post a Comment