MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam jana ilielezwa kuwa Rais mstaafu Benjamin Mkapa ndiye aliidhinisha mchakato wa kuiajiri Kampuni ya Alex Stewart uendelee kwa haraka.
Hayo yalielezwa mbele ya jopo la mahakimu watatu lililokuwa likiongozwa na hakimu John Utamwa wakati Wakili Hurbet Nyange alipokuwa akimhoji shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka Godwin Nyelo (48).
Nyelo ambaye alikuwa Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Sheria na masuala ya Uchumi wa Wizara ya Nishati na madini ni shahidi wa kwanza kwa upande wa mashtaka kutoa ushahidi wake katika kesi ya kutumia madaraka vibaya na kuisababishia hasara ya zaidi ya Sh 11 bilioni serikali inayowakabili Mramba, Daniel Yona na Katibu Mkuu mstaafu wa Wizara ya Fedha na Uchumi Gray Mgonja.
Hata hivyo shahidi huyo alisema Rais Mkapa alihusika katika kukubali mchakato huo uendelee haraka baada ya Wakili Nyange kumuonyesha dokezo na kumtaka asome sehemu ya dokezo hilo naye kufanya hivyo mahakamani hapo.
Dokezo hilo lilikuwa limeandikwa kutoka kwa Daniel Yona ambaye kwa wakati huo alikuwa Waziri wa Nishati na Madini kwenda kwa Rais huyo wa serikali ya awamu ya tatu.
No comments:
Post a Comment