.

.

.

.

Monday, April 19, 2010

YANGA HOI TENA

MECHI ya watani wa jadi, Yanga na Simba iliyochezwa juzi na kumalizika kwa ushindi wa mabao 4-3 wa Simba ilitawaliwa na vituko kadhaa ndani na nje ya uwanja.

Vitendo hivyo ni pamoja na kuanguka na kuzirai kwa shabiki aliyetambulika kwa jina la Hamis Dacota baada ya mwamuzi Mathew Akrama wa Mwanza kuamuru penalti ipigwe kuelekea lango la Simba baada ya kipa Juma Kaseja kumchezea vibaya Abdi Kassim.

Shabiki huyo , mkazi wa Ilala, Dar es Salaam aliondolewa uwanjani hapo na watoa huduma ya kwanza, Chama cha Msalaba Mwekundu kwa machela na kukimbizwa Hospitali ya Temeke ambako alilazwa na kuwekewa driu nne hadi saa 4.00 usiku juzi.

Habari ambazo zilipatikana uwanjani zilieleza Mwananchi kuwa shabiki huyo alianza kujisikia vibaya wakati Simba ikiongoza kwa mabao 3-2 na ilipofika wakati wa mkwaju huo wa penalti wa Jerry Tegete, Dacota alidondoka na kuzimia, bila kushuhudia mkwaju huo uliozaa bao la kusawazisha la Yanga.

Habari ambazo zilizozagaa juzi jijini Dar es Salaam zilidai kuwa shabiki huyo alikuwa amekufa. Lakini, Dacota aliibuka mchana na kuiambia Mwananchi jana kuwa alikuwa salama salimini ila alikuwa akijisikia vizuri kwa matokeo hayo ya 4-3.

Alieleza kuwa alitoka hospitali baada ya matibabu, ingawa bado ana masikitiko ya timu yake kupoteza mechi hiyo.

Mbali na tukio hilo, mwandishi Zaina Malongo anaripoti kuwa shabiki wa Simba katika maeneo ya Mbagala Rangi tatu, Manispaa ya Temeke alitoa mpya baada ya kununua kreti la vinywaji baridi aina ya soda na kuagiza amwagiwe mwili mzima baada ya utabiri wake kwenda sawa kwa Simba itaifunga Yanga.

Shabiki huyo alikwenda kwenye mgahawa ulioko maeneo ya Mbagala na kuwakuta mashabiki na watu wengine kadhaa waliokuwa wakisikiliza mpira uliokuwa ukirushwa hewani na redio na televisheni, zote za Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Baada ya kuwasili mahali hapo, shabiki huyo alimwambia mwenye mgahawa huo, huku wakitaniana kuwa endapo Simba itashinda atanunua kreti nzima kisha amwagiwe pale na kama Yanga ingeshinda mwenye mgahawa angemwagiwa soda hizo.

Baada ya Hillary Echesa kufunga bao na mwamuzi Mathew Akrama kumaliza mchezo huo, shabiki huyo alitoa sh12,000 za krate na kulifungua kisha mashabiki pamoja na mwenye mgahawa huyo walimmwagia soda mchanganyiko akisema anakamilisha furaha yake ya Simba kuifunga Yanga.

Huku akishangilia na mashabiki wenzake wa Simba, shabiki huyo aliondoka na wenzake kumkimbiza mitaani kushangili ushindi huo wa aina yake.

Katika mchezo huo wa kukamilisha ratiba, Simba iliifunga Yanga mabao 4-3 katika mchezo mkali uliofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, ikiwa ni mchezo wa pili kwa Yanga kupoteza katika igi hiyo.

Katika mchezo wa kwanza uliofanyika Oktoba 31, Simba iliifunga Yanga bao 1-0 lililofungwa na Mussa Hassan Mgosi.

SOURCE : MWANANCHI

No comments:

Post a Comment