BINGWA wa mashindano ya soka ya timu za Taifa kwa nchi za Bonde la Mto Nile yanayoanza leo jijini Cairo atazawadiwa zaidi ya Sh milioni 200 za Tanzania. Mashindano hayo yanayoshirikisha nchi saba yatafunguliwa leo kwa mchezo kati ya timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' na Misri 'Farao', pia Burundi itaumana na Uganda. Akizungumza na waandishi wa habari mjini Cairo jana, Rais wa Chama cha Soka cha Misri (EFA), Samir Zahir alisema bingwa atapata pauni milioni moja ya Misri ambayo ni zaidi ya dola za Marekani 176,000 (zaidi ya Sh milioni 200) za Tanzania. "Tumetoa zawadi hiyo kuhamasisha zaidi timu, kucheza kwa nguvu ili kuboresha mashindano yetu ambao ni mara ya kwanza kufanyika," alisema Rais huyo. Pia aliongeza kuwa mshindi wa pili atapata pauni 700,000 za Misri zaidi ya dola 125,000 (zaidi ya Sh milioni 150 za Tanzania), wakati mshindi wa tatu atapata pauni 600,000. "Kutakuwa na zawadi ya mfungaji bora, kipa bora na mchezaji bora, ni aina ya mashindano ambayo tunataka yawe mfano kwa Afrika," alisema Samir. Leo katika mchezo wa Stars na Misri utakaoanza saa mbili usiku kwa saa za Afrika Mashariki, ikiwa ni saa moja kwa saa za huku unatarajiwa kufanyika kwenye Uwanja wa Cairo, ukitanguliwa na mchezo mwingine kati ya Burundi na Uganda, ambapo ratiba ya awali ilikuwa ni Kenya 'Harambee Stars' na Sudan. Ni mtihani wa aina yake kwa Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Mdenmark Jan Poulsen ambaye wino wa kwenye mkataba wake bado haujakauka vizuri tangu awasili nchini Agosti mwaka jana kuanza kibarua cha kuinoa timu hiyo akirithi mikoba ya Mbrazili Marcio Maximo aliyekaa nchini kwa miaka minne. Poulsen mwezi uliopita aliwapa furaha Watanzania kwa kuiongoza timu ya Taifa ya Tanzania Bara 'Kilimanjaro Stars' kuchukua Kombe la Chalenji kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati, michuano iliyofanyika Dar es Salaam. Misri ni mabingwa mara tatu mfululizo wa michuano ya Mataifa ya Afrika, ikiwa imesheheni vipaji tofauti, ambapo kulingana na Kocha Mkuu wa timu hiyo Hassan Shehata kikosi cha Misri kinachoshiriki michuano hiyo ya Mto Nile kina wachezaji 10 waliokuwepo katika kikosi kilichotwaa ubingwa wa Afrika Februari mwaka jana nchini Angola. "Naifahamu Tanzania, nimesikia pia imechukua ubingwa wa Cecafa, si timu ya kubeza, naamini imejiandaa vilivyo, ina wachezaji wazuri na wenye vipaji. "Nawakumbuka wachezaji wawili wadogo walikuwa wakielewana vizuri tulipocheza nao mwaka juzi, kwa ufupi mechi itakuwa ngumu," Shehata aliwaambia waandishi wa habari jana. Stars itaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kubugizwa mabao 5-1 na Misri katika mchezo uliofanyika jijini Aswan Novemba 4, mwaka 2009, kipigo ambacho kilimuweka kwenye wakati mgumu Maximo. Lakini Stars iliyofungwa mabao 5-1 ina tofauti kubwa na hii ambayo leo inatarajiwa kujitupa uwanjani, kuanzia kwa makocha mpaka baadhi ya wachezaji. Wakati huo Stars ilikuwa chini ya Maximo, pamoja na Rodrigo Stokler ambaye alikuwa kocha wa timu za vijana, wakati sasa Stars ipo chini ya Poulsen na Sylivestre Marsh, huku Meneja akiwa yuleyule Leopold Tasso Mukebezi. Ally Mustapha 'Barthez' ndiye alikuwa langoni siku hiyo akishuhudia Waarabu wanavyozifumania nyavu zake, jambo ambalo lililalamikiwa na wadau wengi wa soka kwamba Maximo alimchukua Barthez huku akifahamu hana nafasi katika kikosi chake cha Simba na haikuwa ajabu kufungwa mabao hayo kwani kwa muda mrefu alikuwa hachezi. Kipa aliyekuwa akipigiwa debe na wadau wengi Juma Kaseja, ambaye kipigo hicho cha Stars wengi walimkumbuka, leo ndiyo anatarajiwa kukaa langoni ikiwa ni wiki chache tangu aibuke kipa bora wa michuano ya Chalenji akiwa amefungwa bao moja katika mechi sita alizocheza. Lakini Kaseja naye ana kumbukumbu mbaya na Waarabu kwani Mei mwaka jana, timu yake ya Simba yeye akiwa langoni ilikubali kipigo cha mabao 5-1 kutoka kwa Haras El Hadoud ya Misri mchezo uliofanyika jijini Alexandria katika michuano ya Kombe la Shirikisho. Kaseja atakuwa analindwa na ukuta utakaoongozwa na Aggrey Morris, Nadir Haroub, Stephano Mwasika na 'Babu' Shadrack Nsajigwa, ambapo safu ya kiungo itakuwa chini ya Shaaban Nditi na Nizar Khalfan kuhakikisha wanamdhibiti vilivyo kiungo wa Misri, Mohammed Aboutrika na Ahmed Hassan ambao ni miongoni mwa nyota wa timu hiyo watakaocheza. Washambuliaji wa Taifa Stars wakiongozwa na Mohammed Abdallah a.k.a Machuppa, Saidi Maulidi na Mrisho Ngassa watakuwa na jukumu kubwa la kuipenya ngome ya Misri na kusaka pointi tatu muhimu. "Timu yetu ipo vizuri, nina hakika tutaanza kwa ushindi," alisema Marsh akizungumzia mchezo huo jana. |
.
.
Wednesday, January 05, 2011
KOMBE LA MTO NILE KUANZA JIJINI CAIRO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment