.

.

.

.

Wednesday, February 22, 2012

VIMINI NA KUNYANYUA MAZIWA KUKOMESHWA !!!




KANISA Katoliki limeandaa mpango wa kukomesha uvaaji mbovu unaokwenda kinyume na maadili ikiwamo kuvaa vimini, nguo za kunyanyua matiti na milegezo kanisani baada ya kutangaza kuwavisha vazi la kaniki watakaovaa hivyo.

Matangazo ya kukemea uvaaji mbaya yamekuwa yakitolewa mara kwa mara katika parokia mbalimbali za Jimbo Kuu la Dar es Salaam na mwezi mmoja uliopita, tangazo la kuwavisha kaniki watakaovaa vibaya lilitolewa katika Parokia ya Msewe na vigango vyake.

Taarifa mbalimbali zilizolifikia gazeti hili mapema wiki hii kutoka kwa baadhi ya waumini wa Parokia ya Msewe, ambao hawakuwa tayari kutaja majina yao, zilisema Paroko wao, Piero Clavero na viongozi wa Baraza la Walei, ndio waliotoa tangazo hilo.

“Ni kama mwezi mmoja sasa umepita, Jumapili moja tukiwa kanisani, Paroko alitangaza kukemea uvaaji mbaya na kiongozi mmoja naye akatangaza kuwa Kanisa linaandaa vazi la kaniki ili watakaovaa vimini, milegezo na kuachia matiti kanisani, watavikwa kaniki na wakirudisha watalipia Sh 500 kama fidia,” alisema binti mmoja.

Kauli hiyo pia iliungwa mkono na mwanamke ambaye alidai mara tatu amewahi kuona wasimamizi wawili wa ndoa wanawake wakitolewa nje ya Ibada ya ndoa na kutakiwa kutafuta mitandio baada ya nguo zao kuacha mabega wazi.

Mwenyekiti Msaidizi wa Baraza la Walei, Parokia ya Msewe, Benedict Fungo, alipoulizwa kuhusu tangazo hilo, alikiri kuwa viongozi wa Parokia walitangaza hivyo mwezi mmoja uliopita kwenye misa parokiani na katika kigango cha Kimara-Baruti kwa lengo la kurejesha maadili kanisani.

“Ni kweli tulitangaza, lakini hatukulenga kufukuza watu kanisani, lengo ni kurejesha maadili kwa waumini hasa vijana, unajua kanisani ni nyumba ya Ibada, heshima lazima iwepo, kuna baadhi walikuwa wanakuja wamevaa nguo zinaitwa za kupiga jeki matiti, sasa akienda kupokea Ekaristi (Mwili wa Yesu), padri anakutana na matiti kwanza, tukumbuke hao mapadri nao ni binadamu jamani,” alisema Fungo na kuongeza:

“Sasa ukiwapelekea matiti njenje si unawatamanisha na hii ni dhambi, pia walikuwa wanavaa nguo fupi sana (vimini) na milegezo, mtu akiinama anaacha nguo yote ya ndani nje, haya si maadili yetu, lazima mtoto wako ukiona anakwenda vibaya umkanye, usipofanya hivyo wewe si mzazi mwema”.

Fungo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Liturjia ya Parokia yenye dhamana ya kusimamia maadili, alisema awali miezi miwili iliyopita, walitangaza kuhusu uvaaji kwa maadili na kuzungumza ana kwa ana na baadhi ya waumini hasa vijana walioonekana kuvaa visivyo.

Alifafanua kuwa walifikia uamuzi wa kutoa tangazo hilo si kwa lengo la kuwashitua au kuwafukuza waumini kanisani, bali kuwakumbusha kuhusu maadili na mavazi ya nyumba ya ibada, tofauti na maeneo mengine, ili kujenga nidhamu kama Wakristo lakini pia Watanzania.

Katika kuonesha kuwa tangazo lilifanya kazi, Fungo alisema katika kipindi hicho cha mwezi mmoja, hakuna kijana au muumini aliyekuja kanisani amevaa kihuni; nguo za kunyanyua matiti au fupi na kuwaomba waendelee na heshima hiyo katika nyumba za ibada na hata nje.

“Ukiona baba ananyamaza tu mtoto wake wa kike au wa kiume amevaa nusu uchi, mlegezo au amenyanyua matiti nje ya nguo, huyo si baba mzuri, huwezi kumfukuza mtoto nyumbani kwa uvaaji wake mbovu, lakini unatafuta njia ya kumrekebisha, hiyo ndiyo njia yetu ila hatujamvisha kaniki mtu yeyote mpaka sasa,” alisema Fungo.

Mwenyekiti huyo wa Liturjia alikanusha kufukuza kanisani wasimamizi wa ndoa waliovaa mabega wazi isipokuwa huwa wanaagiza watoto wa mafundisho ya komunyo au kipaimara, wanunuliwe nguo zisizoacha mabega wazi.

Awali Paroko wa Parokia hiyo, Clavero ambaye ni Mzungu anayefahamu vema Kiswahili alipoulizwa na gazeti hili jana kuhusu tangazo hilo alisema: “Mama, mama mama, mama, jamani, hakuna kitu kama hicho, tafadhali hatujatangaza jambo hilo eee.”

Hata hivyo, alipodadisiwa zaidi, alisema baadhi ya watu hawaelewi wala kuheshimu maeneo ya utakatifu, jambo linalodhihirisha kuwapo matangazo hayo parokiani kwake.

Parokia nyingine ambazo baadhi ya watu wamewahi kutolewa nje wakati wa misa hasa za ndoa kwa uvaaji mbovu katika kipindi cha miaka miwili iliyopita ni pamoja na Oysterbay na Kurasini.
 

No comments:

Post a Comment