.

.

.

.

Tuesday, January 01, 2013

MAMA AWACHARANGA KWA MAPANGA WANAE NA KUWAUA


MAMA mmoja mkazi wa Kijiji cha Rhotia wilayani Karatu, anashikiliwa na polisi akidaiwa kuwaua watoto wake wawili kwa kuwachinja kama kuku.
Kwa Karatu, hilo ni tukio la pili kubwa la mzazi kuua wanawe baada ya lile la Mkazi wa Kijiji cha Gekrumu wilayani humo, Evance Damiani (43), kuwaua watoto wake wanne kisha na yeye kujiua kwa kile kilichodaiwa kuwa ni wivu wa mapenzi. Marehemu Damiani aliwacharanga kwa shoka watoto wake, Theophil (11), Ritha (9) na pacha Jigimu na Theodore (6).
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alithibitisha jana kutokea kwa mauaji ya watoto hao na kueleza kuwa uchunguzi bado unaendelea.
“Ni kweli tumepata taarifa hizo kutoka Karatu na uchunguzi wa tukio hilo umeanza ili kujua chanzo cha mama huyo kufanya mauaji hayo,” alisema Kamanda Sabas.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Rhotia, Andrea Mallu alisema jana kwamba mama huyo aliwaua watoto wake usiku wa kuamkia jana.
Mashuhuda waliwataja watoto hao waliochinjwa kuwa ni Mariana Juma (9) mwanafunzi wa darasa la tatu na Patrice Juma (6) anayesoma chekechea.
“Imesemekana kuwa aliwachinja kwa sababu watoto wake walizuiwa kubatizwa na Jumuiya ya Kikatoliki ya Yohanne Mseyi,” alisema mmoja wa mashuhuda hao ambaye hakutaka kutaja jina lake liandikwe gazetini.
Habari zimeeleza kuwa mama huyo sasa anashikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Karatu baada ya kukamatwa na wanakijiji wenzake.
Mallu alidai kuwa mwanamke huyo aliwachinja watoto wake hao wakati bibi yao akiwa katika msiba wa nyumba ya jirani na muda mfupi baada ya kufanya tukio hilo alitoroka.
“Wananchi walishirikiana na kuanza kumsaka na saa 5:00 asubuhi jana walimkuta katika nyumba moja iliyokuwa ikijengwa akiwa amejificha. Alipohojiwa, hakutaka kusema chochote badala yake alitoa karatasi yenye ujumbe kuwa amefanya hivyo baada ya wanajumuiya kukataa kuwabatiza watoto wake.”
Hata hivyo, Mallu alisema kuwa Jumuiya hiyo ya Yohanne Mseyi imekana madai ya mama huyo ikieleza kuwa hakuwahi kuchukua hata fomu zilizokuwa zimetolewa kwa ajili ya ubatizo wa watoto.

No comments:

Post a Comment