Muundo wa Muungano ni kati ya sura za Rasimu ya Katiba ambazo zimezua mjadala mzito kwa wajumbe wa Bunge la Katiba, hasa baada ya kuwapo kwa mgawanyiko wa makundi yenye msimamo tofauti.
Kamati ya Uongozi ya Bunge hilo ilipanga Sura ya kwanza na ya Pili kuwa sura za awali ambazo zitajadiliwa na kamati 12 za bunge hilo, ikiwa ni hatua ya kwanza kabla ya kuingizwa katika mjadala wa Bunge zima.
Mjadala huo ni pamoja na kitendo cha Baraza la Wawakilishi kufanya marekebisho ya katiba yake mwaka 2010 yaliyohusisha kumpa mamlaka zaidi rais wa Serikali ya Mapinduzi na kutangaza visiwa hivyo kuwa nchi, uamuzi ambao umetafsiriwa kuwa ni uvunjaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Hata hivyo, Ismail Jussa anaona kuwa wanaodai matatizo ya Muungano yameanza 2010, wanapotosha.
“Mwaka wa mwanzo wa kuundwa kwa Muungano matatizo yalianza na mgogoro wa mwanzo ulikuja wakati wa utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje,” anasema.
Anasema wakati Zanzibar inaingia katika Muungano, Ujerumani Mashariki ilikuwa ikiitambua na pia Tanganyika ilikuwa ikitambuliwa na Ujerumani Magharibi.
Jussa, ambaye pia ni mwakilishi wa Mji Mkongwe, anasema Ujerumani Magharibi ilikuwa na sera yake kuwa nchi yoyote ambayo itaitambua Ujerumani Mashariki, haitakuwa na mahusiano nayo ya kibalozi.
Anasema baada ya Muungano, kulitokea mgogoro mkubwa baada ya Tanzania kuwa na ofisi mbili za ubalozi. Mgogoro huo uliamuliwa kwa kufungwa kwa ofisi ya ubalozi wa Ujerumani Mashariki.
“Palitokea ugomvi mkubwa kwa kuwa Zanzibar ilikataa kufunga ubalozi wake nchini Ujerumani Mashariki kwa sababu hao ni watu wao na wakati huo tayari walikuwa wameshaanza kuimiminia misaada,” anasema.
Anasema mgogoro huo ulitishia kuvunjika kwa Muungano mwaka 1964, baada ya msimamo huo wa Zanzibar.
“Matokeo yake baada ya mapambano makubwa kwa mara ya kwanza Ujerumani Magharibi, ikawabidi kuvunja historia yao kwa kuruhusu Zanzibar kuendelea kuwa na ofisi Ujerumani Mashariki,” anasema.
Jussa anasema pia mgogoro mkubwa wa sarafu ambao ulijitokeza mwaka 1965 uliohusu Benki Kuu.
No comments:
Post a Comment