

JEETU Patel anayetajwa kuwa kinara wa ufisadi katika wizi wa Sh bilioni 133 kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) pamoja na wenzake tisa, jana walifikishwa mahakamani kujibu tuhuma za kuiibia benki hiyo. Wengine waliofikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam ni Devendra Vinodbhai Patel na Amit Nandy, Ketan Chohan, Johnson Lukaza, Bahati Mahenge, Davies Kamungu, Godfrey Mosha na Manase Mwakale anayeshitakiwa na mkewe, Eddah Mwakale, ambaye ndiye mwanamke pekee katika kesi hiyo ya kifisadi. Jeetu, ambaye jina lake halisi ni Jayantkumar Chandubahi Patel, katika moja ya kesi anazokabiliwa nazo, anashitakiwa kwa pamoja na Devendra Vinodbhai Patel na Amit Nandy. Kwenye shitaka hilo, washitakiwa wanatuhumiwa kula njama, kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo, kuiba na kujipatia Sh bilioni 2.6 kwa kutumia kampuni yao ya Bencon ya Dar es Salaam. Wanadaiwa waliiba fedha hizo baada ya kudanganya kuwa Kampuni ya Matsushita Electric Trading Company iliwapa jukumu la kulipwa fedha hizo kupitia kampuni yao ya Bencon International Ltd. Washitakiwa hao pia kwa pamoja wanashitakiwa kula njama, kughushi, kuiba na kujipatia tena Sh bilioni 7.9 kwa kutumia kampuni hiyo ya Bencon International Ltd. Katika wizi huo, washitakiwa hao wanadaiwa kudanganya kuwa walipewa jukumu la kulipwa fedha hizo na Kampuni ya Maruben Corporation ya Japan wakati wanajua kuwa si kweli. Hakimu Euphamia Mingi alisema dhamana kwa washitakiwa ziko wazi, ila kila mshitakiwa anatakiwa kuweka mahakamani nusu ya fedha anazodaiwa kuiba, wadhamini wawili na mmoja kati yao awe ndugu wa karibu na wote watasaini hati ya dhamana. Washitakiwa hao pia wanatakiwa kuwasilisha hati zao za kusafiria mahakamani, wanatakiwa wasisafiri nje ya mkoa hadi kwa ruhusa ya mahakama. Sharti jingine ni kila Ijumaa ya mwisho wa mwezi wataripoti kwa mwendesha mashitaka na pale wanapokuwa na matatizo, wadhamini wao watalazimika kwenda kutoa taarifa mahakamani. Jeetu pia anashitakiwa katika kesi nyingine na Ketan Chohan na Amit Nandy ambao wanadaiwa kuiba Sh bilioni 3.3 kwa kutumia Kampuni ya Navy Cut Tobacco Tanzania Limited. Walidanganya kuwa wameruhusiwa na Kampuni ya Matsushita Electric Trading Company ya Japan walipwe fedha hizo. Kesi hiyo inasikilizwa na Hakimu Mkazi Neema Chusi na uamuzi wa dhamana yao utatolewa leo. Kinara huyo wa ufisadi, pia anashitakiwa kwa wizi wa Sh bilioni 3.9 ambazo aliiba kwa kutumia kampuni ya Bina Rosorts Ltd kwa kudanganya kuwa walipewa mamlaka ya kulipwa fedha hizo na Kampuni ya C. Itoh & Company Ltd ya Japan. Katika shitaka hilo anashitakiwa kwa pamoja na wenzake Devenra Vinodbhai Patel na Nandy na kesi hiyo iko mbele ya Hakimu Mkazi Richard Kabate. Katika shitaka jingine, Jeetu anashitakiwa kwa wizi wa Sh bilioni 4.9 kwa kushirikiana na Devenra na Nandy. Wote wanatuhumiwa kufanya wizi huo kwa kutumia Kampuni ya Maltan Mining Company Ltd wakidanganya kuwa wameruhusiwa na Kampuni ya Marubeni Corporation ya Japan walipwe fedha hizo na BoT.
WATUHUMIWA WA EPA WAKIWEMO WAFANYABIASHARA JEETHU PATEL NA JOHNSON LUKAZA WAMEFIKISHWA MAHAKAMA YA KISUTU JIJINI DAR LEO WAKIKABILIWA NA MASHITAKA KADHAA KUHUSIANA NA WIZI WA PESA HIZO ZA EPA.
Habari na Picha kwa Hisani ya http://www.issamichuzi.blogspot.com/
WATUHUMIWA WA EPA WAKIWEMO WAFANYABIASHARA JEETHU PATEL NA JOHNSON LUKAZA WAMEFIKISHWA MAHAKAMA YA KISUTU JIJINI DAR LEO WAKIKABILIWA NA MASHITAKA KADHAA KUHUSIANA NA WIZI WA PESA HIZO ZA EPA.Habari na Picha kwa Hisani ya http://www.issamichuzi.blogspot.com/
No comments:
Post a Comment